Sunday, August 26, 2012

AC MILAN WAMKOMALIA KAKA KWA MKOPO, REAL MADRID WASEMA HAKUNA MKOPO, WAKITAKA WAMNUNUE JUMLA!

Kaka
MADRID, Hispania
AC Milan wanajaribu kuishawishi Real Madrid imrejeshe klabuni kwao Mbrazili Kaka kwa mkopo kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi Ijumaa lakini mabingwa hao wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania wanasisitiza kuwa hawako tayari kumuacha kwa mkopo bali kwa kumuuza jumla, makamu wa rais wa Milan,Adriano Galliani amesema leo.

"Hali iliyopo hadi sasa iko wazi: Real wanataka kumuuza Kaka wakati sisi tunamtaka kwa mkopo," Galliani ameiambia Sky Sport.

"Ikiwa Real watabadili msimamo wao, nitakimbilia mara moja kumtwaa lakini kama wakisisitiza kuwa hawamtoi kwa mkopo hatutakuwa na cha kufanya zaidi."

Kocha wa Real, Jose Mourinho amemuacha Kaka nje ya kikosi chake kwa mechi zao zote, ikiwamo ya kwanza ya kuwania taji la Super Cup Alhamisi dhidi ya Barcelona na pia katika kikosi cha leo katika La Liga dhidi ya Getafe, akithibitisha vilevile kuwa mchezaji huyo aliyekuwa Mwanasoka Bora wa Dunia Mwaka 2007 hayuko tena katika mipango yake.

Mabingwa hao wa Hispania wanajaribu kukamilisha usajili wa Luka Modric kutoka Tottenham Hotspur, mchezaji mwenye sifa kama za Kaka, ambaye ameonyesha tu sehemu ya kiwango chake tangu alipotua Real miaka mitatu iliyopita.

Real wanaweza kuwa wagumu kumuacha aende Milan kwa mkopo nyota huyo mwenye miaka 30 kutokana na ukweli kwamba walimnunua kwa klabu hiyo ya Serie A, Ligi Kuu ya Italia kwa euro milioni 65.

Kaka amekuwa pia akihusishwa na uhamisho wa kwenda Paris St Germain, klabu ya Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa inayofundishwea na kocha wake wa zamani katika klabu ya Milan, Carlo Ancelotti.

No comments:

Post a Comment