Wachezaji wa Yanga wakishangilia baada ya kutwaa ubingwa wa Kagame leo jioni. |
Kiungo Rashid Gumbo wa Yanga akimlamba chenga Ibrahim Mwaipopo wa Azam wakati wa mechi yao ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (kombe la Kagame) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni |
Kiungo 'kisheti' wa Yanga, Haruna Niyonzima akipita mbele ya Salum Aboubakar "Sure Boy" (wa pili kulia) na Ramadhani Chombo 'Redondo' (kulia) huku Rashid Gumbo wa Yanga akiwa tayari kumsaidia. |
Lazima utaisoma.... Haruna Niyonzima akimfungisa tela Ibrahim Mwaipopo |
Kipa wa Azam, Deogratius Munishi 'Dida' akiokoa noma langoni mwake |
Niyonzima akijiandaa kumtoka beki wa kati wa Azam, Said Morad |
Beki wa kati na nahodha wa Azam, Aggrey Morris (katikati) akimzuia Said Bahanunzi wa Yanga ili kipa wake Dida adake kiulaini |
Mashabiki wa Azam waliochanganyika na wa Simba wakibeba mfano wa jeneza lenye bendera ya Yanga kabla ya mechi. Hata hivyo baada ya mechi jeneza hilo halikuonekana lilikopitishiwa |
Katika mchezo uliotangulia wa kusaka mshindi wa tatu, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliifunga APR ya Rwanda mabao 2-1. Mabao ya Vita yalifungwa na Magola Mapanda (dk. 18) na Mutombo Kazadi (dk. 67), wakati la kufutia machozi la timu ya APR ya Rwanda lilifungwa na Jean-Baptiste Mugiraneza (dk. 89). Washindi wa tatu Vita wameondoka na dola 10,000. |
Mashabiki wa Yanga wakishangilia bao la kwanza lililofungwa na mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza. |
Mwali huyoooo. Ni raha tu.Wachezaji wa Yanga wakifurahia kombe walilotwaa. |
Kasuku nao walikuwapo kushuhudia mtanange huo huku wakiwa na rangi ya Yanga na bendera ya Yanga. |
Mashabiki wa Azam wakiwa tuliiiiii katika jukwaa la Simba kama wamemwagiwa maji ya baridi baada ya timu yao kupokea kichapo kitakatifu jioni ya leo. |
Bahanuzi ni AK 47..... Shujaa wa bao lililomaliza mechi ya fainali, Said Bahanunzi, akishangilia mbele ya mashabiki wake baada ya mchezo huo kumalizika. |
Ilikuwa ni bonge la pati ya uwanjani. Chezea Yanga wewe....? |
Shujaa wa mabao sita ya Kagame, Said Bahanunzi akishangilia na mashabiki baada ya mechi |
The Big Boss...... Mwenyekiti wa Yanga Yusuph Manji akipita katikati ya uwanja kuwapongeza wachezaji wake baada ya mchezo huo kumalizika. |
Haruna Niyonzima wa yanga (kushoto) akimliwaza winga wa Azam Mrisho Ngassa, ambaye aliingia kutokea benchi huku akiwa ameandika neno AZAM katika nywele zake |
Ilikuwa ni raha tu kwa wana Yanga kwenye Uwanja wa Taifa leo. Picha: sufianimafoto.blogspot.com |
Said Bahanunzi wa Yanga aliondoka na tuzo ya kiatu cha dhahabu kutokana na kufunga magoli sita, sawa na mshambuliaji Taddy Etikiema wa Vita Club ya DRC, lakini nyota huyo aliyetua Jangwani katika kipindi hiki cha usajili akitokea Mtibwa aliibuka na tuzo hiyo kwa sababu mwenzake alifunga goli moja kwa penalti. Hamis Kiiza wa Yanga alifuatia akiwa amefunga magoli matano, huku pasi zake nne alizotoa zikizaa mabao.
Mashujaa wa Yanga katika mechi ya leo walikuwa ni Kiiza aliyefunga goli la kuongoza dakika moja kabla ya mapumziko kufuatia makosa ya beki wa Azam kuzubaa na mpira katika eneo la hatari, na Bahanunzi aliyewamaliza kabisa wageni hao wa michuano kwa goli tamu lilifumua paa la lango lililotokana na beki Said Morad wa Azam kujichanganya na kumuacha mfungaji akiiba mpira na kukimbia nao hadi golini na kufunga katika dakika ya 89.
Azam ambao walitawala dakika 30 za kipindi cha kwanza na 20 za kipindi cha pili walionekana kukosa mbinu za kuuvuka ukuta uliojaa wachezaji wa Yanga ambao walikuwa wakicheza kwa nidhamu ya hali ya juu ya kufuata mipango ya kocha na kuepuka tamaa ya kupanda mbele ovyo hata waliposhambulia.
Beki wa kati na nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro', mlinzi mpya wa kati aliyejiunga akitokea Simba, Kelvin Yondani, beki wa kushoto David Luhende, Stephano Mwasika aliyecheza kama beki wa kulia kutokana na kuumia nyota wa nafasi hiyo Juma Abdul na Godfrey Taita (aliyetolewa kwa kadi nyekundi katika mechi ya nusu fainali), Oscar Joshua na Athuman Idd 'Chuji' kwa muda mwingi wa mchezo walibaki nyuma huku kiungo Chuji akivuka mara chache mstari wa katikati ya uwanja na kufanya "maisha" kwa Azam kuwa magumu sana.
Kiungo wa Azam aliyeng'aa katika michuano hii, Salum Aboubakar 'Sure Boy' mara kadhaa alionekana akiita wachezaji wenzake wajitokeze kutoka katika "msitu" wa walinzi wa Yanga ili awapasie mipira, lakini wingi wa wachezaji wa mabingwa watetezi katika eneo la ulinzi ulikuwa mbinu ngumu kuikabili. Jambo hilo likawalazimu Azam kupiga mashuti kutokea mbali.
Mbinu ya kucheza kinidhamu katika ulinzi ilimfanya mshambuliaji mwenye mabao matano kati ya sita ya jumla waliyofunga Azam katika michuano hii, John Bocco 'Adebayor' kupotea katika msitu wa wachezaji wa Yanga na kushindwa kuisaidia timu yake ambayo goli lao jingine moja pekee lilifungwa Mrisho Ngassa katika mechi ya nusu fainali dhidi ya APR.
Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet, ambaye alikuwa na timu hiyo kwa muda wa wiki moja tu tangu ajiunge nayo, bila ya shaka ndiye alistahili pongezi kutokana na kuibadili timu hiyo iliyoonekana ya kuunga-unga na kuwa timu inayocheza kwa kufuata maelekezo hasa baada ya kipigo cha 2-0 kutoka kwa Atletico ya Burundi katika mechi yao ya ufunguzi ambapo walionekana kuwa timu "nyanya" ambayo katika mechi hiyo ilistahili kufungwa hata magoli 8 kutokana na nafasi nyingi walizotengeneza wapinzani wao, shukrani kwa ushujaa wa kipa aliyekuwa langoni siku hiyo, Mghana Yaw Berko.
Azam licha ya kutawala dakika 30 za kwanza, ni Yanga walioonekana kuwa tishio kila walipofanya mashambulizi yao ya kustukiza kwa kasi kubwa na dakika 15 za mwisho za kipindi cha kwanza zilikuwa ni za Yanga ambao walitawala kwa pasi za uhakika kabla ya makosa ya beki wa Azam, Aggrey Morris kumruhusu Kiiza kuiba mpira na kufunga bao la kwanza.
Kipindi cha pili, Azam walirejea tena na kasi yao kama ya kipindi cha kwanza kwa kutawala mpira, lakini tatizo lilibaki kuwa lile lile -- nafasi ya kupita haikuwepo kwenye "msitu" wa walinzi wa Yanga.
Kuingia kwa Mrisho Ngassa, ambaye alishangiliwa na mashabiki wa Yanga kutokana na kitendo chake cha Alhamisi baada ya nusu fainali cha kuibusu jezi ya wana Jangwani, kuliiamsha Azam katika kipindi cha pili wakati walipokuwa akichukua mipira kutokea wingi yake ya kushoto na kuingia nayo katikati, lakini "msitu" wa walinzi wa Yanga ulimlazimu naye kupiga mashuti ya mbali ambayo mara kadhaa yalipaa juu ya lango.
Mashabiki wa Simba, ambao timu yao ilitolewa na Azam katika robo fainali kwa kipigo cha 3-1, walisahau machungu na kuwashangilia kwa nguvu wana Lambalamba hao wakati wakigongeana pasi, lakini wakati dakika zikiyoyoma huku Yanga wakiwa mbele kwa bao 1-0, mashabi hao wa Msimbazi ambao hata hivyo hawakuwa wengi katika jukwaa lao walianza kuondoka uwanjani na kuzua shangwe kutoka kwa mashabiki wa Yanga.
Usongo wa kupata bao la kusawazisha uligeuka pigo kubwa zaidi kwa Azam pale mshambuliaji aliyejiunga msimu huu akitokea Mtibwa Sugar, Said Bahanunzi, alipofunga goli la pili la Yanga na kuamsha kelele za kufunua paa la juu kutoka kwa mashabiki wa Yanga waliopamba jukwaa lao kwa rangi za jezi zao za njano na kijani.
Wachezaji wa Yanga walimkimbilia kocha wao Saintfiet na kumbeba juu, wakati wengine wakikimbia kushangilia pamoja na mashabiki jukwaani.
Kulikuwa na mashabiki wachache zaidi katika jukwaa la mahasimu wao Simba wakati nahodha Cannavaro alipokuwa akikabidhiwa kombe la tano la michuano hiyo, ambalo sasa ni moja pungufu ya mabingwa wa kihistoria, Simba.
Katika mchezo uliotangulia wa kusaka mshindi wa tatu, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliifunga APR ya Rwanda mabao 2-1. Mabao ya Vita yalifungwa na Magola Mapanda (dk. 18) na Mutombo Kazadi (dk. 67), wakati la kufutia machozi la timu ya APR ya Rwanda lilifungwa na Jean-Baptiste Mugiraneza (dk. 89). Washindi wa tatu Vita wameondoka na dola 10,000.
Mabingwa Yanga waliondoka na dola 30,000 wakati Azam ambao wanastahili kila pongezi kwa kufikia hatua ya fainali katika msimu wao wa kwanza kushiririki, waliondoka na zawadi ya dola 20,000 zinazotolewa na mdhamini wa michuano hiyo Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
No comments:
Post a Comment