KIKOSI
kilichosheheni nyota wapya na yosso waliosajiliwa hivi karibuni cha ‘Wekundu wa
Msimbazi’, Simba kilikosa makali mbele ya lango na kujikuta kikishikiliwa na
Express ya Uganda kwa sare ya 0-0 katika mechi yao ya kujipima nguvu kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Simba ambao wiki
iliyopita walishindwa pia kutambiana na Express katika mechi yao waliyocheza
mjini Shinyanga na kutoka sare ya 1-1, walionyesha kandanda safi tangu mwanzo
wa mechi na kutawala kwa gonga zao safi katika muda mwingi wa mchezo.
Kiungo Mussa
Mudde aliyetua kwa ‘Wanamsimbazi’ akitokea katika klabu ya Sofapaka ya Kenya
alikaribia kuifungia Simba bao la mapema katika dakika ya pili tu baada ya
kukaribia lango na kupiga shuti ambalo hata hivyo lilidakwa na kipa Didi
Mohamed wa Express.
Katika dakika ya
tisa, Mudde alikaribia tena kufunga baada ya kupata nafasi nzuri lakini shuti
lake likatoka nje ya lango.
Simba
waliendelea kuonana na kukosa bao jingine katika dakika ya 23 kufuatia gonga
safi za Uhuru Selemani na Christopher Edward kumaliziwa vibaya na Shomari
Kapombe aliyepiga shuti lililopaa.
Wageni
walipoteza pia nafasi nzuri ya kufunga katika dakika ya 30 baada ya
mshambuliaji Jingo Slyman kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa William
Mweta wa Simba. Timu zote zilishambuliana kwa zamu katika kipindi cha pili na
kukosa nafasi kadhaa za kufunga, hasa Simba ambao mara kadhaa walilikaribia
lango la Express lakini mashuti ya yosso wao hayakuwa na madhara.
Simba wataondoka
leo kuelekea Zanzibar kushiriki mashindano ya Kombe la Urafiki ambapo watashuka
dimbani leo usiku kucheza dhidi ya Mafunzo ambapo mahasimu wao Yanga watakwenda
pia Zanzibar kushiriki mashindano hayo kujiandaa na michuano ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) itakayofanyika Dar es Salaam kuanzia
Julai 14.
No comments:
Post a Comment