Baadhi ya anafunzi jijini Dar wakiandamana leo kutaka serikali imalize mgomo wa walimu ili nao wapate nafasi ya kuendelea na masomo yao |
Wanafunzi wakiwa katika maandamano ya kuunga mkono walimu wao jijini Dar es Salaam leo. |
"Tunataaaaka.... haki yeeetu". Baadhi ya wanafunzi wakiandamana jijini Dar es Salaam leo kuunga mkono walimu wao. |
Baadhi ya wanafunzi jijini Dar es Salaam wakiwa nje ya madarasa baada ya walimu wao kugoma. |
Kama ilivyokuwa katika maeneo kama ya Tunduma mkoani Mbeya, baadhi ya wanafunzi wa jiji la Dar waliandamana na kuelekea katika ofisi mbalimbali za serikali zinazoshughulikia elimu huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kuwaunga mkono walimu wao ambao wameanza mgomo leo wakitaka serikali iwalipe stahili zao mbalimbali.
Miongoni mwa wanafunzi waliojimwaga mitaani kupinga hatua ya serikali ya kutowasikiliza walimu na kusababisha mgomo ni baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi za maeneo ya Mbagala na Mbezi ambako mabasi yaendayo mikoani yalikuwa na wakati mgumu kuendelea na safari zao.
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kupitia kwa rais wao, Gratian Mukoba, kilitangaza kuanza kwa mgomo mkubwa wa walimu wa nchi nzima leo ili kuishinikiza serikali iwatekelezee madai yao mbalimbali.
Hata hivyo, Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Elimu, Phillip Mulugo ilipinga mgomo huo kwa kusema kuwa ni batili na pia ikawaonya walimu kuwa yeyote atakayeshiriki atahesabiwa kuwa ni mtoro kwani mgogoro wao hivi sasa uko mahakamani.
KAULI YA WAZIRI WA ELIMU KAWAMBWA
Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa, amewataka walimu kuacha mgomo wao mara moja na kurejea madarasani kuendelea kufundisha kwani wanawakosesha wanafunzi haki yao ya kikatiba ya kupata elimu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq amewaagiza wakurugenzi wa manispaa za jiji la Dar es Salaam kuwabaini walimu wote waliogoma leo na wale waliofika shuleni na kusaini daftari la mahudhurio bila kufundisha ili wachukuliwe hatua kali.
RUVUMA, MBEYA
Hali kama ya jiji la Dar es Salaam ilitokea pia katika ameneo mengi nchini ikiwa ni pamoja na mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Iringa, Morogoro na kwingineko nchini.
Chama cha walimu (CWT) kimesema kuwa mgomo wao umeanza kwa mafanikio makubwa leo kwani karibu asilimia 80 ya walimu waliuunga mkono na kutoingia madarasani.
Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo, walimu waliendelea kufanya kazi zao kama kawaida, huku wakisema kuwa hawaoni sababu ya kufanya mgomo ambao unawaumiza zaidi watoto wasiokuwa na hatia.
No comments:
Post a Comment