Mhe. George Mkuchika, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) |
Idara ya
Usalama wa Taifa imekanusha taarifa zinazowahusisha na tukio la kutekwa,
kuteswa na kumtupa kwenye msitu wa Mabwepande jijini Dar es Salaam kiongozi wa
Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka.
Taarifa
iliyotolewa leo na idara hiyo imeeleza kuwa habari zinazodai kwamba ndio
waliohusika kumteka Dk. Ulimboka ambaye hivi sasa anaendelea na matibabu nchini
Afrika Kusini na nyingine zinazodai kuwa wana mpango wa kuwadhuru watu
mbalimbali si za kweli, na kwamba wanaozisambaza wana lengo la kuichafua
taasisi hiyo nyeti kwa usalama wa taifa.
Kwa sababu
hiyo, taarifa hiyo imewataka wananchi kupuuza taarifa hizo, na kuwahakikishia
Watanzania kuwa 'uzushi' huo hautawavunja moyo.
Imeeleza
zaidi kwamba badala yake, Idara ya Usalama wa Taifa itaendelea kushirikiana na
wananchi na vyombo vingine vya usalama katika kuhakikisha kuwa wakati wote nchi
inakuwa salama.
Taarifa hiyo
imetolewa leo ikiwa ni siku moja tu baada ya gazeti la Mwanahalisi la jana Jumatano
(Julai 25, 2012) kuwatuhumu watu wa usalama wa taifa kuhusika na tukio la
kumteka Dk. Ulimboka.
Katika habari
hiyo, Mwanahalisi liliwataja kwa majina baadhi ya watu waliodaiwa kuwa ni maafisa
wa idara hiyo waliohusika kumteka Dk. Ulimboka.
Dk. Ulimboka
aliyekuwa mstari wa mbele katika harakati za mgomo wa madaktari uliotokea hivi
karibuni, alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana na kuumizwa vibaya kabla ya
kukutwa kwenye msitu wa Mbawepande.
Kamanda wa
Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Slaam, Suleiman Kova alimtaja Mkenya
Joshua Mhindi kuwa ndiye mtuhumiwa aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo,
akieleza kwamba walimtia mbaroni baada ya kubaini kuwa alikwenda katika Kanisa
la Wokovu na Uzima la Mchungaji Gwejima lililopo Kawe jijini Dar es Salaam kwa
nia ya kuungama huku akikiri kufanya tukio hilo na wenzake wa kundi la Gun Star.
Idara ya
Usalama wa Taifa iko chini ya Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala
Bora), ambayo inaongozwa na Mhe. George Mkuchika.
No comments:
Post a Comment