Monday, July 30, 2012

TUNDU LISSU AFICHUA MAJINA YA WABUNGE ALIODAI NDIO WANAOTUHUMIWA KWA RUSHWA/KUTETEA MASLAHI BINAFSI

*YUMO PIA MBUNGE WA SIMANJIRO, CHRISTOPHER OLE SENDEKA

Mhe. Tundu Lissu
Mhe. Ole Sendeka
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Mhe. Tundu Lissu, amefichua majina ya wabunge anaodai kwamba ni miongoni mwa wale wanaotuhumiwa kujihusisha na rushwa au kujaribu kutumia ushawishi wao kwa maslahi yao binafsi.

Akizungumza mjini Dodoma leo, Mhe. Lissu aliwataja watuhumiwa hao ambao wote wanatoka CCM, na ambao awali walikuwemo kwenye Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika Anna Makinda mwishoni mwa wiki kutokana na kashfa hiyo kuwa ni:

1. Sara Msafiri
2. Charles Mwijage
3. Munde Abdallah 

4. Mariam Kisanga
5. Christopher Ole Sendeka
6. Vicky Kamata

Hivi karibuni, Bunge lilijikuta likipata msukosuko mkubwa baada ya baadhi ya wabunge kutuhumiwa kupokea rushwa ili watumiwe kwa maslahi ya wafanyabiashara wa mafuta.

Ilidaiwa kwa kutumia nguvu za rushwa au kupigania maslahi yao binafsi kwa vile walikuwa wakinufaika na uongozi uliowekwa kando wa TANESCO, baadhi ya wabunge walipania kuikaanga Wizara ya Nishati na Madini, hasa katibu mkuu wake Eliakim Maswi.

Ilielezwa kwamba sababu kubwa ni uamuzi wa Wizara ya Nishati wa kuzinyima tenda kampuni nyingine tenda ya kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya UPTL na badala yake kuipa kazi hiyo kampuni ya Puma, ambayo pia inamilikiwa na serikali kwa asilimia 50.

Hata hivyo, orodha hiyo ya Mhe. Lissu ambaye pia ni mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni haikumtaja mbunge yeyote wa chama chake (CHADEMA), licha ya uvumi kuzagaa kuwa nacho kina wabunge wake wanaotuhumiwa pia kujihusisha na rushwa.

Katika maelezo yake, Mhe. Lissu aligusia baadhi ya tuhuma za wabunge hao, huku akimtaja Mhe. Sara Msafiri kuwa ndiye anayejihusisha kufanya biashara na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) , sawa na Mhe. Mwijage.

Mhe. Lissu alidai kuwa waheshimiwa Abdallah na Mariam Kisanga wana vituo vya mafuta na Mhe. Ole Sendeka alimtuhumu kuwa ndiye mtetezi mkuu wa makampuni yaliyonyimwa na serikali tenda ya kuiuzia mafuta IPTL.

Mbunge huyo alidai kwamba wameambiwa kwamba kwa Mhe. Kamata kuna mgongano wa kimaslahi, mambo ambayo hata hivyo alidai kwamba si vizuri sana kuyasema.   

No comments:

Post a Comment