![]() |
Mhe. Sugu |
![]() |
Kamanda Kova |
![]() |
Mchungaji Gwejima |
Dk. Ulimboka akiwa hospitali |
Akizungumza
bungeni jioni hii wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya
Wizara ya Mambo ya Ndani, Mhe. Sugu alisema kuwa taarifa alizotoa Kova akidai kwamba
kuna mtu (Mkenya Joshua Mhindi) alikwenda kuungama kwa mchungaji, ni filamu
ambayo haijaeleweka kwa wananchi na kwamba, anamshauri Kamanda Kova arudi tena
studio ili kuiandaa upya.
“Ni
filamu ambayo haijaeleweka kwa wananchi… hivyo warudi tena studio,” alisema Sugu
kabla Spika wa Bunge, Mhe. Anna Makinda kuingilia kati na kumtaka mbunge huyo akae
chini kwani dakika zake za kuchangia hoja ya wizara hiyo zilikuwa
zimeshamalizika.
Hivi
karibuni, Kamanda Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa polisi wamemkamata raia
wa Kenya, Joshua Mhindi (31) baada ya mtu huyo kwenda Kawe, katika Kanisa la
Ufufuo na Uzima la Mchungaji Josephat Gwejima na kwa nia ya kuungama kwamba alihusika
kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka huku akiwa na wenzake wa kikundi cha Gun Stars.
Hata
hivyo, wakati wa ibada ya juzi Jumapili, Mchungaji Gwejima alikanusha baadhi ya
maelezo yaliyotolewa na Kamanda Kova, ikiwemo madai kuwa Mkenya huyo alikwenda kuungama
kwenye kanisa lao, huku pia akielezea hofu yake kuwa huenda mtu huyo (Mhindi) alitumwa
au anasumbuliwa na matatizo ya akili.
Kwa
mara nyingine, Kamanda Kova aligusia suala hilo jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusema kuwa hayuko tayari kumjibu Mchungaji
Gwejima kwavile suala hilo limeshafikishwa kortini na hivyo kulizungumzia nje ya utaratibu wa chombo hicho ni
sawa na kuingilia uhuru wa mahakama.
Dk.
Ulimboka alikuwa mstari wa mbele wakati wa mgomo wa madaktari uliofanyika
nchini hivi karibuni kabla hajakumbwa na kadhia ya kutekwa na watu
wasiojulikana ambao walimteka na kumtesa vibaya kabla ya kumtupa katika msitu
wa Mabwepande jijini Dar es Salaam. Hivi sasa Dk. Ulimboka anaendelea na
matibabu nchini Afrika Kusini.
TAHADHARI
YA SUGU
Awali,
katika mchango wake huo, Mhe. Sugu aliitaka Serikali kuweka hadharani matokeo ya uchunguzi
wa tume iliyoundwa baada ya vurugu za wamachinga zilizotokea Novemba 11 ambapo
watu kadhaa walipigwa risasi za moto na wengine kupata ulemavu, akiwemo mtu
mmoja ambaye alidai kuwa hivi sasa ana hali mbaya na anasubiri kuwekewa nyonga ya
bandia.
Alisema
kuwa watu wa jimboni kwake (Mbeya Mjini) hawatakuwa tayari kumpokea kiongozi
yeyote wa serikali ikiwa uchunguzi wa tume hiyo haujawekwa wazi.
Mhe. Sugu
pia aliwatahadharisha watu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, akiwataka wawe makini
katika kazi zao na kuhakikisha kuwa wanatanguliza weledi na kamwe wasikubali kutumiwa.
Alisema
kuwa wizara hiyo ni nyeti katika nchi yoyote ile, na kwamba historia inaonyesha
kuwa wale wanaokwenda na maji na watawala huwa ni watu wa namna yao na wala si
wanajeshi, huku akitaja mfano wa yaliyotokea Misri, Algeria na Iraq.
No comments:
Post a Comment