![]() |
Maradona |
![]() |
Bruno Metsu |
KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Senegal na Umoja wa Falme za Kiarabu, Bruno Metsu amerithi nafasi ya kocha aliyetimuliwa, Diego Maradona katika kuifundisha klabu ya Al Wasl, klabu hiyo ya Dubai imesema katika taarifa yake leo.
Muargentina Maradona (51), ambaye aliwahi kutwaa Kombe laDunia akiwa na timu ya taifa lake, alitimuliwa wiki iliyopita huku akiwa amebakiza mwaka mmoja kumaliza mkataba wake wa miaka miwili baada ya kumaliza msimu bila kuipa Al Wasl taji lolote.
"Taarifa zaidi zitatolewa kwenye mkutano na waandishi wa habari ambao utafanyika siku chache zijazo wakati wa kumtambulisha rasmi Metsu kuwa kocha mkuu," ilisema klabu hiyo katika taarifa yake iliyotolewa kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, ambayo ilieleza vilevile kuwa Mfaransa Metsu, 58, amesaini mkataba wa miaka miwili.
Maradona alitimuliwa baada ya Al Wasl kumaliza katika nafasi ya nane kwenye UAE Pro League, Ligi Kuu ya UAE yenye timu 16, ikishuka kwa nafasi mbili zaidi kulinganisha na ilivyomaliza msimu uliopita.
Klabu hiyo pia ‘ilichemsa’vibaya katika kuwania makombe mawili ya nyumbani na pia haikufuzu kwa michuano ijayo ya Ligi ya Klabu Bingwa Asia.
Metsu aliiongoza timu ya taifa ya UAE kutwaa ubingwa wa taji la Gulf Cup 2007 wakati alipoiongoza kwa miaka mitatu, na pia aliiongoza Senegal kwenye fainali za Kombe la Dunia 2002, ambako waliwafunga Ufaransa waliokuwa mabingwa wa Dunia kwa bao 1-0 katika mechi yao ya ufunguzi kabla ya kufika robo fainali ya michuano hiyo.
Metsu pia ni kocha pekee aliyewahi kuipa timu ya UAE taji la Ligi ya Klabu Bingwa Asia, akifanya hivyo wakati akiiongoza Al Ain mwaka 2003.
No comments:
Post a Comment