Monday, July 9, 2012

KOCHA NEWCASTLE AMNG’ANG’ANIA DEMBA BA

Demba Ba  

NEWCASTLE, England
KOCHA wa Newcastle, Alan Pardew ameelezea dhamira yake ya kuhakikisha kuwa straika Demba Ba haondoki katika klabu yake.

Baada ya kuanza msimu wake wa kwanza vizuri ambapo straika huyo wa timu ya taifa ya Senegal alifunga mabao 16 katika michuano yote, kumekuwa na uvumi unaomhusisha Ba na uhamisho utakaomtoa kwenye klabu yake ya sasa.

Mchezaji huyo wa zamani wa West Ham ana kipengele katika mkataba wake kinachoweza kumuondoa kirahisi klabuni hapo baada ya kufikia mwisho wa mwezi huu, na klabu ya Galatasaray ya Uturuki inatajwa kuwa ni moja ya timu nyingi zinazomfukuzia.

Lakini Pardew amepuuza uvumi huo, na kusisitiza kwamba Ba mwenye miaka 27 atakuwa ni miongoni mwa wachezaji watakaoongoza safu yao ya ushambuliaji wakati msimu mpya wa Ligi Kuu ya England utakapoanza Agosti 18.

"Nataka Demba abaki," Pardew aliiambia Sky Sports.
"Ni mchezaji wa Newcastle na kitu pekee ninachoangalia ni kuhakikisha kwamba anendelea kuwa mchezaji wa Newcastle msimu ujao."

Klabu hiyo itapigania kumaliza katika nafasi nne za juu msimu ujao baada ya msimu uliopita kutwaa nafasi mojawapo ya kushiriki Ligi ya Europa, na Pardew anajua kwamba kikosi kilichojaa vipaji kinahitajika kukabiliana na shinikizo.

"Matarajio yatakuwa makubwa msimu ujao, na ninakubaliana na hali hiyo," aliongeza. 

"Tulipambana na timu kubwa msimu wote uliopita na tunapaswa kupata tena mafanikio kama hayo mwakani."

No comments:

Post a Comment