Sunday, July 15, 2012

HAYE AMDUNDA KIRAHISI CHISORA KWA 'KO'

David Haye akimshuhudia Dereck Chisora "akilamba sakafu" wakati alipomchapa kwa KO katika raundi ya tano usiku huu. 

BINGWA wa zamani wa dunia wa uzito wa juu, David Haye, amemdunda kirahisi kwa KO ya raundi ya tano mpinzani wake Dereck Chisora, katika pambano lililomalizika hivi punde lililosubiriwa kwa hamu kubwa kufuatia utata wa vibali uliozunguka mabondia hao waliofungiwa kupigana na mamlaka za ngumi.


Haye alitawala pambano hilo tangu mwanzo akionekana kupigana kwa kujiamini na ilimchukua Chisora hadi raundi ya tatu kurusha ngumi ya kwanza ya maana usoni mwa Haye.


Chisora (kushoto) akipokea ngumi kutoka kwa Haye

Chisora (kushoto) akiwa amelewa ngumi mfululizo, anaanza kuelekea chini.
Shughuli imeisha.... Chisora akienda sakafuni

Chisora ambaye kabla alimwaga tambo nyingi ikiwemo kudai kwamba "ataingia katika pambano hilo kama kichaa" na kwamba atamdondosha Haye katika raundi ya saba, alikuwa ni yeye aliyeenda chini mara mbili katika raundi ya tano na mchezo kuishia hapo.


Ngumi mbili -- ya kulia na ya kushoto -- chini ya shavu la huku na kule, zilimlambisha sakafu Chisora kwa mara ya kwanza mapema katika raundi ya tano lakini aliinuka baada ya kuhesabiwa.


Muda mfupi baada ya kuruhusiwa kuendelea na pambano, Haye hakutaka kumpa muda wa kurejea katika hali yake ya kawaida, akamfuata haraka na kuendelea kushambulia. Ngumi tano mfululizo zilizoingia kwenye taya na usoni zilimpeleka chini Chisora ambaye wakati akijaribu kuinuka, refa alimaliza pambano.


Kwa ushindi huo, Haye aliongeza rekodi ya mapambano yake kuwa ameshinda 26 (24 kwa KO) na amepigwa mawili hajatoka sare, wakati Chisora sasa amepigwa mara 4, ameshinda 15 (9 kwa KO) na hajatoka sare.


Haye mwenye urefu wa futi 6 na inchi 3, ametwaa mataji mawili ya Kimataifa ya WBO na WBA ya uzito wa juu kutokana na ushindi huo. Lilikuwa ni pambano lake la kwanza kurejea ulingoni tangu alipopigwa na Vladimir Klitschko Julai 2011 na kupoteza mkanda wake wa dunia wa WBA na kutangaza kustaafu.

No comments:

Post a Comment