Monday, July 2, 2012

DK. ULIMBOKA ‘AMPONZA’ MBUNGE MOSES MACHALI


Mhe. Moses Machali
Mbunge wa Kasulu Mjini kupitia NCCR-Mageuzi, Mhe. Moses Machali, ametolewa nje ya ukumbi wa Bunge na Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba baada ya kuibuka majibizano makali kuhusiana na sakata la mgomo wa madaktari na kupigwa kwa Dk. Steven Ulimboka.

Tukio hilo limetokea jioni ya leo (muda mfupi uliopita) wakati wa mjadala unaoendelea kuhusiana na makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kwa mwaka ujao wa fedha.

Awali, mchangiaji aliyekuwa akijadili hoja hiyo, Mhandisi Stella Manyanya alitoa shutuma dhidi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa kinahusika na migomo inayoendelea ya madaktari.

Hata hivyo, Mbunge wa Ubungo, Mhe.  John Mnyika alisimama na kutaka Mhe. Manyanya athibitishe hoja yake kwani yeye akiwa kiongozi wa chama hicho,  hafahamu kikao chochote walichokaa ili kuratibu migomo.

Kabla Mnyika hajamaliza, naye alitoa rai ya kuitaka Serikali kuwasilisha bungeni ripoti ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kuhusiana na madai ya madaktari ambayo alidai ingesaidia kukomesha propaganda zinazotolewa na Serikali kuhusiana na mgomo huo.

Hatua hiyo ikaibua mabishano zaidi baada ya Mbunge wa Iramba, Mwigulu Mchemba kusimama na kutoa taarifa kuwa CHADEMA wamethibitisha namna wanavyounga mkono mgomo wa madaktari kupitia hotuba yao ya kambi ya upinzani (akinukuu kuanzia ukursa wa 21); aliyodai kuwa inaunga mkono watumishi wa serikali wanaodai haki zao.

Wakati majibizano yakiendelea, Mhe. Machali alisimama na kutaka kuzungumza. Mwenyekiti Mabuma hakumruhusu Machali na kumtaka mbunge huyo aka echini, lakini Machali aliendelea kusimama na ndipo Mwenyekiti (Mabumba) akaamuru askari wa Bunge kumuondosha ukumbini humo, kisha  Mhe. Manyanya akaendelea kuchangia.

No comments:

Post a Comment