Didier Deschamps, kocha mpya wa timu ya taifa ya Ufaransa, akifurahi wakati wa mkutano mkuu wake wa kwanza katika makao makuu ya shirikisho la soka la Ufaransa mjini Paris leo (Julai 9, 2012). |
Didier Deschamps (kushoto) akisimamia mazoezi wakati akiifundisha Olympique Marseille mjini Marseille, Septemba 19, 2011. Picha: REUTERS |
PARIS, Ufaransa
DIDIER Deschamps ametajwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Ufaransa jana Jumapili, akiwa nyota mwingine wa kikosi kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka 1998 kupewa jukumu gumu la kuwaweka pamoja nyota waliojaa malumbano kuwa timu yenye umoja na mafanikio kulingana na ukubwa wa vipaji vyao.
"Noel Le Graet, rais wa Shirikisho la Soka la Ufaransa, na Didier Deschamps wamemaliza majadilano yao na wamefikia maafikiano ya kumteua Bwana Deschamps kuwa kocha wa Ufaransa," taarifa ya FFF ilisema.
Mkutano wa kumtambulisha kwa wanahabari utafanyika leo saa 8:30 mchana kwenye makao makuu ya shirikisho hilo.
Nahodha huyo aliyeiongoza Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1998, aliondoka Olympique Marseille wiki moja iliyopita na anachukua mikoba ya Laurent Blanc, ambaye alijiuzulu kufuatia timu hiyo ya taifa kutolewa katika robo fainali ya Euro 2012.
Kazi ya kwanza ya Deschamps itakuwa ni kuiunganisha timu yenye mpasuko mkubwa wakati wakijaribu kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil kutokea kwenye kundi gumu linalowajumuisha mabingwa wa dunia Hispania.
Shirikisho hilo limewafungulia mashitaka wachezaji wanne, akiwemo Samir Nasri ambaye alimbwatukia maneno machafu mwandishi wa habari, kwenye kamati maadili kutokana na "tabia mbaya" kwenye Euro 2012.
Blanc, ambaye alichukua timu hiyo mwaka 2010 baada ya aibu iliyowakumba ya kutolewa kirahisi kwenye Kombe la Dunia, aliondoka baada ya timu yake kuonyesha kiwango kidogo katika mechi waliyolala 2-0 na waliokuja kuwa mabingwa Hispania kwenye fainali za Mataifa ya Ulaya zilizofanyika Ukraine na Poland.
Blanc alitafakari kwa muda kama asaini mkataba mpya na kisha akaamua kujiuzulu, huku ripoti za vyombo vya habari zikisema klabu kubwa za Ulaya zinamhitaji.
Deschamps, ambaye rekodi zake za ukocha pia ni za "kupanda na kushuka", pia alihitaji siku kadhaa kabla ya kufikia maamuzi ya kuikubalia ajira hiyo.
Alioongoza timu ndogo ya Monaco kutinga fainali za Klabu Bingwa Ulaya mwaka 2004 na akairejesha Juventus kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mwaka 2007 kufuatia kushushwa daraja kutokana na kashfa ya kupanga matokeo lakini akajiuzulu baada ya kutofautiana na bodi kuhusu usajili wa wachezaji wapya.
Marseille ilitwaa ubingwa wa Ufaransa mwaka 2010 chini ya utawala wake kama kocha lakini msimu uliopita ulikuwa mbaya kwa timu hiyo ya Ufaransa yenye mashabiki wengi zaidi wakimaliza katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligue 1.
Mechi yake ya kwanza madarakani kwa timu ya taifa ya Ufaransa itakuwa ni ya kirafiki dhidi ya Uruguay mjini Le Havre Agosti 15.
No comments:
Post a Comment