Tuesday, July 31, 2012

CHRISTOPHER OLE SENDEKA AMSHITAKI TUNDU LISSU

Mhe. Christopher Ole Sendeka

Mhe. Tundu Lissu

Mbunge wa Singida Mashariki, Mhe. Tundu Lissu, ameshtakiwa leo mbele ya Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge kwa kosa la kuwatuhumu wabunge kadhaa wa CCM kuwa ndio wanaojihusisha na rushwa, akiwamo Mbunge wa Simanjiro, Mhe. Christopher Ole Sendeka.


Akizungumza bungeni leo, Spika wa Bunge, Mhe. Anna Makinda, alisema kwamba Tundu Lissu atatakiwa ajieleze mbele ya kamati hiyo na kutoa ushahidi wake huko kutokana na tuhuma alizotoa jana dhidi ya Ole Sendeka na wabunge wengine, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.


Awali, Ole Sendeka alisimama na kuomba mwongozo wa Spika baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, akihoji kama ibara ya 100 inayozungumzia kinga ya wabunge inaweza kumpa nafasi ya kulifikisha suala hilo mahakamani kwani amedhalilishwa kwa hatua ya hatua ya jana ya Tundu Lissu kumtaja yeye na wabunge wengine kadhaa mbele ya waandishi wa habari kuwa ndio wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa bungeni.


Baada ya kuomba mwongozo huo leo, ndipo Spika Makinda alipoamuru kwamba Tundu Lissu apelekwe katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge ili akajieleze kwavile ibara ya 100 inamlinda asipelekwe mahakamani kwa vile alisemea mambo hayo akiwa katika eneo la kumbi za Bunge. 
Spika akasema kuwa Lissu atakuwa shahidi wa kwanza kuhojiwa na kamati aliyoipa jukumu la kuchunguza suala hilo na hivyo atatakiwa kuwasilisha ushahidi wa tuhuma alizotoa dhidi ya Ole Sendeka na wabunge wengine aliowataja.    


Akieleza zaidi, Mhe. Makinda akawasisitiza wabunge kuwa wawe na subira juu ya tuhuma zinazoendelea kufanyiwa kazi na kamati ya uongozi wa bunge kuhusiana na madai kuwa baadhi ya wabunge hujihusisha na rushwa na wengine kutumia wadhifa wao katika kupigania maslahi binafsi bungeni.

Chanzo cha sakata hilo ni kubainika kuwa baadhi ya wabunge wamekuwa wakipokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wa mafuta ili wawatetee bungeni baada ya kukosa tenda ya kuliuzia Shirika la Umeme (TANESCO) mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL.

Wizara ya Nishati na Madini ilikabidhi tenda hiyo ya kuiuzia mafuta TANESCO kwa kampuni ya Puma, ambayo pia inamilikiwa na serikali kwa asilimia 50.

Wabunge wengine wamedaiwa kupigania zaidi maslahi yao kwani hufanya biashara na TANESCO na hivyo wakawa wakitumia ushawishi wao kuishambulia Wizara ya Nishati na Madini, hasa katibu mkuu wake Eliakim Maswi ambaye hivi karibuni alitangaza kumtimua Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO na vigogo wengine kadhaa kwa tuhuma ubadhirifu.

Tundu Lissu aliwataja wabunge aliodai kuwa ndio wanaotuhumiwa kwa kashfa hiyo kuwa ni Christopher Ole Sendeka, Sara Msafiri, Charles Mwijage, Munde Abdallah, Mariam Kisanga  na Vicky Kamata.

Wabunge wote aliowataja Tundu Lissu wanatoka CCM, na awali walikuwamo kwenye Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika Anna Makinda mwishoni mwa wiki kutokana na kashfa hiyo ya baadhi ya wajumbe wake kutuhumiwa kwa rushwa.

 

No comments:

Post a Comment