Monday, August 20, 2012

MBWANA SAMATTA AACHA GUMZO KUBWA MISRI... NI BAADA YA KUZIPIGA MABAO ATAKAVYO KLABU ZAO VIGOGO ZA ZAMALEK NA AL AHLY.... SASA ABAKIZA GOLI MOJA TU KUWASHIKA ABOUTRIKA NA TRESOR MPUTU.....!

Samatta akipiga mahesabu ya kumtoka beki wa Zamalek

Goooooooooooohhh.....! Chezea Samatta wewe.... hapa 'dogo' anafunga bao la pili lililoing'oa Zamalek katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika jana.

Huyu dogo noma sana. Sijui kaja ni vizizi vyake kutoka kwao Mbagala? Kipa wa Zamalek akiwa hoi baada ya kupigwa bao 'kali' na Samatta.

Aiya weee.... basi tena! Kipa wa Mazembe akijutia baada ya kushindwa kuokoa mpira wa kichwa cha Samatta jana. 
CAIRO, Misri
STRAIKA wa kimataifa wa Tanzania amezua gumzo kubwa nchini Misri baada ya jana kuendeleza rekodi yake ya kuzipiga mabao klabu vigogo za nchi hiyo wakati alipofunga goli kali la kichwa na kuipa timu yake ya TP Mazembe ushindi wa 2-1 dhidi ya Zamalek kwenye uwanja usio na mashabiki jijini Cairo nchini humo.

Chanzo cha gumzo la Samatta miongoni mwa mashabiki wa soka nchini Misri ni uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira, kuwatoka mabeki na kutumia vyema nafasi anazopata katika kufunga, hasa katika mechi tatu zilizopita za ligi ya klabu bingwa Afrika ambapo klabu yake ilicheza dhidi ya klabu vigogo nchini humo za Al Ahly na Zamalek.

Kabla ya mechi ya jana, Samatta aliwasumbua sana mabeki wa Al Ahly na kufunga kwa kichwa bao pekee la Mazembe wakati klabu yake ikilala 2-1 katika mechi ya kundi lao la B iliyochezwa nchini Misri. Wiki mbili zilizopita, Samatta aliwapelekesha kadri alivyotaka mabeki wa Zamalek ambao ni mahasimu wa jadi wa Ahly na kufunga bao mojawapo kali la kichwa wakati wakishinda nyumbani 2-0.

Na jana tena, Samatta alikuwa ni mmoja wa nyota wa Mazembe waliowanyima raha mabeki wa Zamalek na kuwakosakosa zaidi ya mara mbili kabla ya kupiga goli 'tamu' la kichwa liliwapa ushindi wa 2-1 na kuing'oa Zamalek katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Rekodi hiyo ya muda mfupi, akipiga magoli matatu kwa kichwa katika mechi tatu zilizopita dhidi ya klabu vigogo za Misri, ndio chanzo cha mjadala wa Samatta nchini Misri.

Katika mechi ya jana usiku iliyochezwa kwenye uwanja usio na mashabiki kwa sababu za kiusalama, nahodha wa Mazembe, Tresor Mputu ndiye 'aliyetengeneza' mabao yote ya Mazembe.

Kona ya Mputu katika dakika ya 34 iliunganishwa vyema kwa kichwa kilichopigwa na Mzambia Hichani Himoonde na kuwapa wageni bao la utangulizi. Dakika moja baadaye, Zamalek wakasawazisha kupitia kwa nyota wa kimataifa wa Benin, Razak Omotoyossi, ambaye aliudokolea wavuni mpira wa krosi ya chini kutoka wingi ya kushoto uliotoka kumpita kipa veterani, Robert Kidiaba.

Samatta aliifungia Mazembe bao la ushindi kwa kuunganisha vyema krosi nzuri ya Mputu wakati zikiwa zimebaki dakika chache kabla ya mapumziko.

Bao hilo la jana, sasa limemfanya Samatta afikishe jumla ya mabao matano katika michuano hiyo na kuendelea na kasi nzuri ya kufukuzia kiatu cha dhahabu, akibakiza goli moja tu kuwashika nyota Tresor Mputu wa klabu yake ya Mazembe na Mohamed Aboutrika wa Ahly ambao kila mmoja amefikisha mabao sita huku megine yakitokana na penati. Mghana Emmanuel Clottey wa Berekum Chelsea ya Ghana yuko kileleni mwa orodha ya wafungaji baada ya kufunga mabao 12 huku matatu yakitokana na penati.

Kufuatia ushindi wa jana, Mazembe wamefikisha pointi saba na kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo, pointi tatu nyuma ya Al Ahly wanaoongoza kundi lao la B. Chelsea ya Ghana inaifuatia Mazembe baada ya kufikisha pointi tano na Zamalek inaburuza mkia kwa kutokuwa na pointi huku kila timu ikiwa imebakiza mechi mbili kumaliza mechi za hatua ya makundi.

Ahly ilishikiliwa na Chelsea kwa sare ya 1-1 mjini Accra jana na baada ya kuwahi kuongoza kwa tofauti ya pointi tano wiki mbili zilizopita, sasa hawana tena uhakika wa kumaliza kileleni mwa kundi hilo, ingawa tayari wameshajihakikishia nafasi ya pili na kutinga nusu fainali.


Vinara wa ufungaji Klabu Bingwa Afrika:
                                                                       Magoli      Penati
Emmanuel Clottey    (Berekum Chelsea)        12              3
Mohamed Aboutrika  (Al Ahly)                        6               2  
Tresor Mputu            (TP Mazembe)                6               1
Mbwana Samata       (TP Mazembe)                 5               0
Isu Azuka                 (Sunshine)                        5               0
      

ALEX SONG ATUA MJENGONI BARCELONA... WENGER ASEMA INAUMA LAKINI SIO ISHU SANA KWAVILE ARSENAL INA VIUNGO KIBAO KAMA DIABY, WILSHERE, ROSICKY…!


Yaap, hapa nilipotua nd'o penyewe... ntapata umateumate wa ukweli na makombe ntabeba mpaka makwapa yaniume! Kiungo Alex Song akipozi kwa picha leo ndani ya mjengo wa Barcelona nchini Hispania.  
Alex Song akiwa kwenye mjengo wa klabu ya Barca leo asubuhi.

Mzukaaaaa....! Mbwembwe za Alex Song baada ya kutua kwenye mjengo wa Barca leo.
BARCELONA, Hispania
Kiungo aliyekuwa Arsenal, Alex Song anatarajiwa kusaini mkataba wake wa kuichezea Barcelona kwa miaka mitano baada ya kutambulishwa rasmi leo katika tukio la kuchukuliwa kwa vipimo vya afya.


Kiungo huyo wa kimataifa wa Cameroon mwenye miaka 24, yuko mbio kusaini mkataba huo baada ya klabu yake ya Arsenal kukubali ‘dili’ la kumuuza kwa paundi za England milioni 15 (Sh. bilioni 37)

Taarifa iliyotolewa leo na Barca imeeleza kuwa baada ya kusaini mkataba wake, kiungo huyo atatambulishwa mbele ya waandishi wa habari kesho.

Song hakucheza juzi Jumamosi katika mechi ya Arsenal ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Sunderland iliyomalizika kwa sare ya 0-0, na baadaye Arsenal kuthibitisha kuwa wamekubali kumuuza kiungo huyo kwa Barca.

"Siku zote huwa inauma kupoteza wachezaji wazuri, lakini tuna wachezaji wengi katika eneo la kiungo," alisema kocha wa Arsenal, Arsene Wenger.

"Tunaangalia pia uwezekano wa kuleta kiungo mwingine mmoja, na pengine beki mwingine mmoja pia kwa sababu tunadhani kwamba bado tuna upungufu katika baadhi ya maeneo," alisema Wenger, huku taarifa zikidai kwamba wanamfukuzia kiungo asiye na nafasi katika klabu ya Real Madrid, Nuri Sahin.

Miongoni mwa viungo kibao ambao Wenger anajivunia ndani ya kikosi chake cha Arsenal ni pamoja na Abou Diaby, Jack Wilshere, Tomas Rosicky na Santi Cazorla aliyemsajili msimu huu akitokea Malaga.

Song, aliyekuwa amebakiza miaka miwili kumaliza mkataba wake, alijiunga na Arsenal wakati akiwa na miaka 17 akitokea katika klabu ya Bastia ya Ufaransa mwaka 2005.

Awali alitua kwa mkopo wa mwaka mmoja, kisha akapewa mkataba wa kudumu baada ya kutwaliwa jumla kwa ada ya paundi za England milioni 2.75 (Sh. bilioni 7)

Hivi karibuni, Arsenal pia waliwasajili mastraika Olivier Giroud na Lukas Podolski, lakini vilevile wakimpoteza nahodha wao Robin van Persie waliyemuuza kwa Manchester United kwa ada ya paundi za England milioni 24 (Sh. bilioni 60).

BOTI NYINGINE YAZAMA ZANIZIBAR IKITOKEA TANGA LEO, WATU 10 WAOKOLEWA, WENGINE WASAKWA... INAITWA MV. SARWAK

Ilivyokuwa boti ya Mv. Skagit baada ya kupinduka katika eneo la Chumbe na baadaye kuzama yote... hapa, baadhi ya abiria wakisubiri kuokolewa wakati ikiwa bado haijazama yote kwenda chini kwa umbali wa kina cha zaidi ya mita 60. Tukio hili lilijiri Julai 18.
Boti ndogo iitwayo Mv. Sarwak iliyokuwa ikisafiri kati ya Tanga na Zanzibar imezama leo na hadi sasa watu 10 wameokolewa na kukimbiziwa hopspitali visiwani humo huku wengine wawili wakiwa hawajulikani waliko.

Taarifa kutoka Zanzibar zimeeleza kuwa tayari msako dhidi ya watu hao wawili unaendelea na kwamba, majeruhi wako katika eneo la Vikokotoni visiwani humo.

Imeelezwa kuwa raia wawili kutoka Uholanzi na mmoja wa Ufaransa ni miongoni  mwa abiria 10 walionusurika baada ya kupatiwa 'life jacket' kabla ya kuzama kwa chombo hicho na baadaye kuokolewa.

Kwa mujibu wa manusura, boti hiyo ndogo ilizama baada ya pampu zake zinazotumika kuondoa maji kuharibika ghafla na hivyo maji kujaa wakati ikiendelea na safari kati ya eneo la Pangani, Tanga na Vikokotoni, Zanzibar.

Tukio hilo lililojiri leo limekumbushia ajali kubwa zaidi iliyotokea Julai 18 wakati meli ya Mv Skagit iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Zanzibar ilipozama katika eneo la Chumbe na kusababisha vifo vya abiria wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 200.

BILA NYIE ISINGEWEZEKANA... VILLA AREJEA ATUPIA, MESSI APIGA 2, BARCA YAUA 5-1, REAL YASHIKWA 1-1, RONALDO HOI...

Mshambuliaji wa Barcelona, David Villa akishangilia goli lake alilofunga dhidi ya Real Sociedad kwa kuonyesha fulana yake yenye picha ya familia yake, inayosomeka: "Bila ya nyie isingewezekana", ambapo alikimbilia kuwakumbatia madaktari wa timu hiyo kwenye Uwanja wa Nou Camp mjini Barcelona jana usiku Agosti 19, 2012. Villa, ambaye alikaa nje ya uwanja kwa tangu alipovunjika mguu Desemba mwaka jana, aliruhusiwa kucheza na madaktari wa Barca mwezi uliopita. Picha: REUTERS

Mshambuliaji wa Barcelona, David Villa akishangilia goli lake alilofunga dhidi ya Real Sociedad kwa kuonyesha fulana yake yenye picha ya familia yake, inayosomeka: "Bila ya nyie isingewezekana", ambapo alikimbilia kuwakumbatia madaktari wa timu hiyo kwenye Uwanja wa Nou Camp mjini Barcelona jana usiku Agosti 19, 2012. Villa, ambaye alikaa nje ya uwanja kwa tangu alipovunjika mguu Desemba mwaka jana, aliruhusiwa kucheza na madaktari wa Barca mwezi uliopita. Picha: REUTERS
Lionel Messi akiwafungisha tela wachezaji wawili wa Real Sociedad wakati wa mechi yao ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Hispania kwenye Uwanja wa Nou Camp mjini Barcelona jana usiku Agosti 19, 2012. Messi alitupia mbili, Puyol moja, Pedro moja na David Villa moja.
Dah mambo haya yakiendelea tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia ntaipata kweli... Straika wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo akijiuliza baada ya kupoteza nafasi ya kufunga wakati wa mechi yao ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) dhidi ya Valencia kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid jana usiku Agosti 19, 2012. Real walitoka 1-1, huku goli la Real likifungwa na Higuain. Picha: REUTERS

Mastraika wa Real Madrid, Gonzalo Higuain (kushoto) na Karim Benzema wakitoka uwanjani baada ya mechi yao ufunguzi wa Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Valencia kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid jana usiku Agosti 19, 2012. Real walianza kutetea ubingwa wao wa La Liga kwa fadhaa baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Valencia, licha ya kutawala mechi nzima kwenye Uwanja wa Bernabeu. Picha: REUTERS
Kipa wa Real Madrid, Iker Casillas akisikitika wakati wa mechi yao ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) dhidi ya Valencia kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid jana Agosti 19, 2012. Real walitoka 1-1, huku goli la Real likifungwa na Higuain. Picha: REUTERS

Kocha wa Valencia, Mauricio Pellegrino (kushoto) akimsalimia kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho kabla ya mechi yao ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Valencia kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid jana usiku Agosti 19, 2012. Real walianza kutetea ubingwa wao wa La Liga kwa fadhaa baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Valencia, licha ya kutawala mechi nzima kwenye Uwanja wa Bernabeu. Picha: REUTERS