Tuesday, November 6, 2012

KATIBU WA MUFTI ZANZIBAR, SHEIKH SORAGA AMBAYE ALIMWAGIWA TINDIKALI LEO ASUBUHI SASA ALAZWA KATIKA WODI YA WAGONJWA MAHUTUTI KWENYE HOSPITALI YA TAIFA YA MUHIMBILI… RAIS KIKWETE AMJULIA HALI…!

Rais Kikwete akimjulia hali Sheikh Soraga aliyelazwa ICU kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili leo Novemba 6, 2012..
Pole Sheikh sana...! Rais Kikwete akimjulia hali Sheikh Soraga aliyelazwa ICU kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili leo Novemba 6, 2012.
Mbebe kwa uangalifu... Sheikh Soraga akibebwa kuwahishwa Muhimbili.
Harakati za kumuwahisha Sheikh Soraga Muhimbili akitokea Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar. 
Hapa Sheikh Soraga akianza kutolewa na gari la wagonjwa kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar kupelekwa Uwanja wa Ndege kabla ya kukimbiziwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.


Katibu wa Mufti Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga amelazwa ICU katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  jijini Dar es Salaam akiwa hoi baada ya kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana katika eneo la Magogoni Msumbiji Mkoa wa Mjini Magharibi mjini Zanzibar leo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, amekwenda kumpa pole Sheikh Soraga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kumtakia kheri ili apone haraka.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai,Yussuf Ilembo, amesema wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya  Jeshi la Polisi, Ziwani Zanzibar kuwa Sheikh Soraga ameimwagiwa tindikali leo alfajiri wakati akifanya mazoezi binafsi ya viungo.

Ilembo alisema wakati akiendelea na mazoezi, alimuona mtu mwingine akifanya mazoezi mbele yake kabla mtu huyo hajamgeukia na kumwagia tindikali iliyomjeruhi vibaya sehemu za usoni na kifuani.

Baadaye mtu aliyefanya unyama huo alitoweka na kuelekea kusikojulikana.

Ilembe alisema tayari uchunguzi umeanza kufanyika na Jeshi la Polisi litahakikisha linatumia nguvu zake zote kuwasaka wahusika.

Sheikh Soraga alifikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Zanzibar lakini baadaye, kwa mujibu wa  Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Dk. Jamala Adam Taib, walilazimika kumkimbizia jijini Dar es Salaam ambako alipelekwa kwa ndege iliyotolewa na serikali na kufikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.

Wakati akisafirishwa kutoka Zanzibar, Sheikh Soraga alibebwa katika gari la wagonjwa aina ya  Toyota (Na. DFP 5049),  kisha  akapakiwa katika ndege ya serikali yenye namba 5H-TGF Tanzania, mishale ya saa 3:45 asubuhi kupelekwa Dar es Salaam na kusindikizwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali iddi.

Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Kabi, aliwataka wananchi kuwa na subira kufuatia tukio hilo.

Alisema Zanzibar inaweza kuingia katika maafa makubwa iwapo watu watapoteza subira na uadilifu na kwamba wasipokuwa makini, wanaweza kujitumbukiza katika maafa makubwa kama ilivyokuwa katika nchi nyingine barani Afrika kama Rwanda.

Vyama vya CCM na CUF vinavyoongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar cimelaani vikali tukio hilo na kutaka uchunguzi mkali ufanywe ili wahusika wafikishwe mbele ya mkono wa sheria.

“Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano kwa polisi ili kuwafichua watu wanaohusika na iovu kama huu,” amesema Naibu Katibu Mkuu wa CUF upande wa  Zanzibar,  Salim Bimani.

No comments:

Post a Comment