Geofrey Nyange 'Kaburu' akiwa katika kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Maunga kilichopo Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam leo . PICHA: SANULA ATHANAS |
MSHAMBULIAJI Mganda Emmanuel Okwi alikuwa kivutio leo kwa watoto, vijana hadi wazee waliokuwa wakigombea kupiga picha naye wakati klabu yake ya Simba ilipotembelea kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Maunga Centre cha Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam.
Okwi, ambaye juzi alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Simba katika tamasha la klabu hiyo la Simba Day, aligombewa na mashabiki kituoni hapo ambapo watoto kwa wazee walitaka japo kupeana naye mikono au kupiga picha naye.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema wakati akizungumza na viongozi wa kituo hicho kuwa klabu yake imeanzisha utaratibu wa kuwa karibu na jamii na imeanzisha wiki maalum iitwayo 'Simba Week', ambayo itakuwa ikifanyika kila mwaka kuanzia Agosti 5-10.
Alisema Wiki ya Simba itakuwa ikihusisha nyota na viongozi wa klabu hiyo kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwamo kutembelea watu wenye mahitaji ambayo itakuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Simba Day. Siku ya Siomba hufanyika Agosti 8 kila mwaka.
Katika ziara hiyo Simba ilitoa msaada wa mchele Kg.310, mafuta ya kupikia lita 100, dawa za meno, sabuni na fedha taslimu Sh. 500,000 kwa ajili ya kusaidia watoto wanaolelewa kituoni hapo.
Juzi Jumanne, Simba walifanya ziara kama hiyo katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam na kutoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa hasa wodi ya akinamama na wajawazito.
No comments:
Post a Comment