Michael Carrick akiwa katika jezi itakayotumiwa na Man United msimu huu. |
Alex Oxlade-Chamberlain akiwa katika uzi mpya ambao Arsenal itauvaa msimu huu... naye ameitwa taifa England |
KIUNGO wa Manchester United, Michael Carrick amerejeshwa katika kikosi cha timu ya taifa ya England kinachojiandaa na mechi ya kirafiki itakayopigwa Jumatano dhidi ya Italia.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 aliomba kutofikiriwa tena katika majukumu ya kitaifa Januari, baada ya kuachwa nje ya kikosi kilichoenda kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini.
Lakini kutokana na kukosekana kwa Scott Parker na Gareth Barry kutokana na kuwa majeruhi, Carrick amerejeshwa katika kiungo pamoja na Frank Lampard.
Jake Livermore, Ryan Bertrand, Steven Caulker na Tom Cleverley nao pia wamejumuishwa.
Kocha Roy Hodgson amefanya mabadiliko kadhaa, ambapo Steven Gerrard, John Terry na Wayne Rooney wakiwa miongoni mwa waliopumzishwa.
England itashusha uwanjani safu ya ulinzi iliyojaa sura ngeni kwani pia Ashley Cole, Joleon Lescott na Glen Johnson wote wameachwa.
Beki wa Chelsea, Gary Cahill, ambaye alikosa fainali za Euro 2012 kutokana na kuvunjika taya, amerejeshwa, pamoja na beki wa Tottenham, Kyle Walker, ambaye alikosa michuano hiyo kutokana na majeraha.
Mshambuliaji wa Liverpool, Andy Carroll amejumuishwa licha ya giza kutawala kuhusu hatma yake ya klabu, wakati winga wa Arsenal, Theo Walcott pia ameitwa miongoni mwa wachezaji wa mbele.
Frank Lampard, ambaye pia alikosa Euro 2012 kutokana na majeraha, amejumuishwa lakini ni kurejeshwa kwa Carrick ndiko kulikoshangaza wengi.
Kiungo huyo wa United hajajihusisha na timu ya taifa ya England kwa miaka miwili na aliomba kutofikiriwa katika kikosi cha Euro 2012 kutokana na kutopewa nafasi mara kwa mara katika timu yake ya taifa.
Mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham, ambaye mwaka 2001 ndio alicheza mechi ya kwanza kati ya mechi zake 22 alizochezea taifa lake, amekuwa "akifumbiwa macho" na kikosi cha timu ya England licha ya kutwaa makombe manne ya Ligi Kuu ya England na moja la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika miaka sita akiwa Old Trafford.
Mwezi uliopita, Carrick alidokeza kwamba atakuwa tayari kurejea timu ya taifa kama kocha Hodgson atamwita.
"Hakutaja kufikiriwa kwa ajili ya Euro, hivyo nikadhani kwamba watu wasiotaka hawako tayari," alisema Hodgson.
"Alizungumza na Gary (Neville) na mimi baadaye na imeonyesha kwamba anataka kucheza.
"Hapajawahi kuwa na shaka kwamba Carrick hakuwa mawazoni mwetu ama mipango yetu. Lakini ilikuwa ni suala la kuamini kwamba hakuwa tayari kuichezea tena England."
Carrick ni mmoja wa wachezaji wazoefu wachache katika kikosi kilichojaa vijana wakati Hodgson akijaribu kuwweka mizani sawa ya matakwa ya klabu ya kujiandaa na msimu mpya huku naye akijiandaa na mechi hiyo itakayochezwa Uswisi.
Chama cha soka cha England (FA) kimesisitiza kwamba kuachwa kwa Terry hakuhusiani na nahodha huyo wa Chelsea kuwa na kesi ya ubaguzi dhidi ya Anton Ferdinand katika kamati ya nidhamu ya chama hicho.
FA ilishaweka wazi wakati ilipomfungulia mashitaka Julai 27 kutokana na tuhuma hizo kwamba bado atakuwa huru kuchezea England.
Kikosi kamili cha timu ya taifa ya England:
Makipa:
Joe Hart (Manchester City), Jack Butland (Birmingham City), John Ruddy (Norwich City).
Mabeki:
Leighton Baines (Everton), Ryan Bertrand (Chelsea), Gary Cahill (Chelsea), Steven Caulker (Tottenham Hotspur), Phil Jagielka (Everton), Kyle Walker (Tottenham Hotspur).
Viungo:
Michael Carrick (Manchester United), Tom Cleverley (Manchester United), Frank Lampard (Chelsea), Adam Johnson (Manchester City), Jake Livermore (Tottenham Hotspur), James Milner (Manchester City), Alex Oxlade-Chamberlain (Arsenal), Jack Rodwell (Everton), Ashley Young (Manchester United).
Washambuliaji:
Andy Carroll (Liverpool), Jermain Defoe (Tottenham Hotspur), Daniel Sturridge (Chelsea), Theo Walcott (Arsenal).
No comments:
Post a Comment