Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiq |
Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Said
Mecky Sadiq, amewaagiza wakurugenzi wa manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni
kuwaandikia barua za kuwataka kujieleza walimu wote waliokosekana kwenye vituo
vyao vya kazi jana katika siku ya kuanza kwa mgomo usio na kikomo uliotangazwa
na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Akizungumza na waandishi leo, mkuu
huyo wa mkoa alisema kuwa mgomo huo si halali na kwamba, walimu wote waliouunga
mkono watachukuliwa hatua.
Akitoa tathmini ya mahudhurio ya
walimu jana, Sadiq alisema kuwa hali haikuwa mbaya sana katika shule za msingi
kulinganisha na sekondari.
Alisema kwamba katika Manispaa ya
Temeke, walimu walioshiriki mgomo jana ni 1,484 ambao ni sawa na asilimi 34,
Kinondoni waligoma walimu 2,074 na waliogoma Ilala ni walimu
107 tu, ambao ni sawa na asilimia
5.95.
NAIBU WAZIRI PHILLIP MULUGO
Naibu Waziri wa Elimu na na
Mafunzo ya Ufundi, Phillip Mulugo, alifanya ziara ya ghafla mkoani Morogoro na
kuangalia athari za mgomo katika baadhi ya shule, zikiwamo za sekondari Morogoro,
sekondari Kilakala na Shule ya Msingi Mwere.
Naibu Waziri huyo alikuta walimu
45 wa sekondari Morogoro wamegoma na alipofika katika shule ya Mwere, alikuta
wanafunzi wengi wakiwa nje ya madarasa baada ya walimu kukosekana madarasani.
Hata hivyo, Mulugo alikuta walimu
wa shule ya Kilakala wakiendelea na kazi kama kawaida huku katibu wa Tawi la CWT
shuleni hapo akisema kuwa wao hawaungi mkono mgomo huo.
Jana, walimu nchini walianza
mgomo usio na kikomo uliotangazwa na CWT kwa nia ya kuishinikiza serikali kuwatekelezea
madai yao kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwaongezea mishahara kwa asilimia 100.
No comments:
Post a Comment