Kaka |
MADRID, Hispania
REAL Madrid haina mpango wa
kumruhusu Kaka kujiunga na AC Milan kwa mkopo wa mwaka mmoja na badala yake
wanataka kumuuza jumla, gazeti la Marca limeripoti.
Milan ambao ni vigogo wa Serie A,
Ligi Kuu ya Italia wamepania kumrejesha kiungo huyo nyota wa kimataifa wa
Brazil katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, na tayari wameshazungumza na
wakala wa mchezaji huyo kujadili uwezekano wa kumsajili.
Hata hivyo, hali ngumu ya kifedha
waliyo nayo Milan inakwaza dhamira yao, na klabu hiyo ina matumaini ya
kumsajili Kaka kwa mkopo bila kulipia ada ya uhamisho, huku pia wakiiomba Real
kuendelea kumlipa asilimia 50 ya mshahara wa kiungo huyo.
Real hawautaki mpango huo na
badala yake wako tayari kumruhusu aondoke kwa mkataba wa kudumu.
Mazungumzo baina ya klabu hizo
yataendelea katika siku zijazo, na Real ambao ni mabingwa wa La Liga, Ligi Kuu
ya Hispania, watasisitiza kwamba Milan ni lazima waonyeshe dhamira ya kweli ya
kumhitaji Kaka kabla ya kuendelea na majadiliano yao.
No comments:
Post a Comment