Tuesday, July 24, 2012

UBOVU VIWANJA VYA SOKA WACHEFUA WABUNGE


Juma Semsue wa Polisi Dodoma akibebwa na wenzake baada ya kufunga goli katika mechi mojawapo ya ligi kuu msimu uliopita kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.  

Sehemu ya Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambao hivi sasa unalalamikiwa kwa kuharibika vibaya kwenye eneo   
Hali mbaya ya viwanja vingi vya soka nchini vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) inaendelea kuwakera wabunge na baadhi yao wameitaka serikali kuvirejesha mikononi mwake kwani vinahatarisha usalama wa wachezaji na hata mashabiki wanaofika kushuhudia mechi mbalimbali za mchezo huo.

Wabunge wameyasema hayo leo asubuhi na mchana wakati wa kuchangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya ya mwaka wa fedha 2012/13 ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo huku wakiutaja uwanja wa Jamhuri Dodoma kuwa ni mfano wa viwanja hivyo vibovu kabisa na vinavyohatarisha usalama wa watumiaji wake.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Mhe.Grace Kiwelu, amesema sasa ni wakati mwafaka kwa CCM kufanya uamuzi wa busara wa kuvirudisha viwanja hivyo serikalini kama ilivyofanya kwa shule za sekondari zilizokuwa zikiendeshwa na Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho.

Akitolea mfano Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Mhe. Kihwelu alisema: “Umekuwa na hali mbaya kiasi ambacho hata wabunge wanaofanya mazoezi wapo hatarini kuumia viungo vyao.”

Alisema uwanja huo ambao upo katika makao makuu ya serikali na pia chama tawala (CCM), hauna hadhi ya kuitwa uwanja baada ya nyasi zake za kuchezea kutoweka na baadhi ya majukwaa kuvunjika.Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), alisema viwanja vinavyomilikiwa na CCM kwa sasa havijiendeshi kibiashara na ndiyo maana vimechakaa kupita kiasi, hivyo serikali ichukue hatua ya kuvihudumia.

"Tunaomba serikali ivihudumie viwanja
hivi kwa sababu havijiendeshi kibishara, vipo kwa ajili ya kutoa huduma tu na ndiyo maana vinachakaa," alisema.

Viwanja vingine vya soka vilivyo aktika hali mbaya hivi sasa na baadhi kumilikiwa na CCM ni CCM Kirumba Mwanza, Ali Hassan Mwinyi Tabora, Jamhuri Morogoro, Majimaji Songea, Mkwakwani Tanga, Lake Tanganyika Kigoma,Umoja Mtwara, Samora Iringa, Sheikh Amri Abeid Arusha na Kambarage wa Shinyanga.

MAISHA PLUS YAREJEA KATIKA TV YAKO

Masoud Kipanya, mratibu wa shindano la Maisha Plus

Abdul kutoka Zanzibar, mshindi wa kwanza wa Maisha Plus 1

Steven Sandhu, alifika fainali ya Maisha Plus 1

MSIMU wa tatu wa mashindano ya maisha halisi ya katika televisheni ya Maisha Plus 2012 umeanza huku usaili wa kwanza kwa ajili ya kupata washiriki 21 watakaoingia katika kijiji cha mashindano ukipangwa kufanyika Agosti 3.

Masoud Kipanya, mratibu wa shindano hilo, ambaye pia ni mkurugenzi wa DMB Company Ltd inayoandaa Maisha Plus, alisema jijini Dar es Salaam jana mashindano hayo yatahusisha washiriki kutoka mikoa 13 na kwamba usaili utaanza Arusha Agosti 3, Moshi Agosti 4 na kisha Tanga utafanyika Agosti 5.

Mikoa mingine itakayofanyika usaili huo ni Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mtwara, Zanzibar na Dar es Salaam.

Moja ya mambo mapya katika Maisha Plus 2012 ni kwamba itakuwa na uhusiano na shindano la Mama Shujaa wa Chakula.

Mama Shujaa wa Chakula ni shindano linaloandaliwa na shirika la Oxfam. Shindano hili huwashindanisha wanawake wanaojihusisha na kilimo kidogo. Limewahi kufanyika mwaka jana na mshindi alikuwa ni Ester Jerome kutoka Dodoma, ambaye alijishindia zawadi ya trekta.

Unaweza kujiuliza "ni vipi Maisha Plus 2012 itashirikiana na Mama Shujaa wa chakula?", Masoud anajibu kwamba washiriki wa Mama Shujaa wa Chakula wataingia kijijini kabla ya vijana wa Maisha Plus, ambako watakaa kwa wiki mbili mpaka mshindi mshindi wao atakapopatikana. Baada ya hapo watatoka na ndipo shindano la Maisha Plus litakapoanza rasmi.

Alisema majaji wa Maisha Plus 2012 watakuwa ni Kaka Bonda, yeye mwenyewe Masoud Kipanya na Baby Madaha na kwamba shindano litaonyeshwa kila siku TBC1.

Kipanya aliongeza kuwa vigezo vya ushiriki ni umri baina ya miaka 21-26, awe Mtanzania bila ya kuzigatia rangi, elimu ya sekondari, mbunifu, ana ujuzi wa mawasiliano na mchapakazi.

Katika msimu wa kwanza wa Maisha Plus uliofanyika mwaka 2009, kijana Abdulhalim Hafidh wa Zanzibar aliibuka na mshindi na ilipofanyika kwa mara ya pili mwaka 2010, Alex wa Mbeya alishinda.

BOTI PACHA YA MV SKAGIT IITWAYO MV KALAMA YAPIGWA STOP ZANZIBAR


Mv Kalama
Mv Kalama inavyoonekana kabla ya kupigwa stop kubeba abiria na Serikali ya Zanzibar leo
Mv Skagit inavyoonekana baada ya kupinduka chini juu na baadhi ya abiria wake wakisubiri kuokolewa kabla ya kuzama yote baharini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Iddi
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza kuiipiga marufuku boti ya Mv Kalama inayofanana kwa kila hali na boti iliyozama wiki iliyopita na kuua mamia ya watu ya Mv Skagit baada ya kubaini kuwa haifai kusafirisha abiria kwa umbali mrefu.

Boti hiyo, ambayo pia inamilikiwa na kampuni ya Seagull Transport Sea Company Limited kama ilivyokuwa Mv Skagit, sasa haitaruhusiwa kujihusisha kabisa na biashara ya usafirishaji wa abiria katika visiwa hivyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, alithibitisha juu ya uamuzi huo wa serikali leo wakati akipokea mchango wa Sh. milioni 10 kwa ajili ya wahanga wa ajali ya kuzama kwa Mv Skagit  kutoka kwa Shirika la Mfuko wa Ustawi wa Jamii (NSSF) na kukabidhiwa na mkurugenzi wa mfuko huo, Dk. Ramadhani Dau. 

Jana, serikali ya Zanzibar iliunda tume ya kuchunguza sakata la kuzama kwa Mv Skagit katika eneo la Chumbe wakati ikitokea Dar es Salaam kwenda Zanzibar huku ikiwa na watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 340.

Tayari aliyekuwa waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, Hamad Masoud Hamad ametangaza kujiuzuku kutokana na tukio hilo ambalo limeibua maswali mengi kwani taarifa zilizopo, na ambazo sasa zimethibitishwa kutokana na uamuzi uliotangazwa na Balozi Iddi, zinadai kwamba boti hizo (iliyozama ya Skagit na Mv Kalama) ziliengenezwa kwa ajili ya kufanya kazi kama vivuko tu, zikitakiwa kutembea umbali mfupi.

KADA CCM AKUTWA LEO NA HATIA WIZI WA FEDHA ZA EPA, AFUNGWA MIAKA MITATU

Maranda (kulia) na Farjala.

Farjala (kushoto) na Maranda (mbele kushoto) wakisindikizwa katika korido za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imewahukumu kwenda jela miaka 18 wafanyabiashara na ndugu wawili, Rajabu Maranda ambaye alikuwa mweka hazina wa CCM mkoani Kigoma na Farijala Hussein, baada ya wote kupatikana na hatia ya makosa sita kati ya saba waliyokuwa wanakabiliwa nayo, yakiwemo ya kujipatia Sh bilioni 2.2 za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Licha ya kutakiwa kwenda jela miaka 18, watatumikia miaka mitatu jela ambayo itakwenda sambamba pamoja na kifungo cha awali cha miaka mitano kutokana na kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa, ambayo ni kula njama, kughushi nyaraka, kuwasilisha hati bandia na kujipatia Sh. 2,266,049,041.25.

Mahakimu  waliosikiliza kesi hiyo walikuwa na hukumu mbili tofauti. Ya kwanza iliandaliwa na Mwenyekiti wa jopo la mahakimu hao, Fatuma Masengi ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu aliyepewa kibali na Jaji Mkuu Tanzania kusikiliza kesi hiyo ambaye aliona washtakiwa hao hawana hatia.


Hukumu nyingine iliyotumika na mahakama imeandaliwa na mahakimu wawili, Projestus Kahyoza na Katalina Revocat -- hii iliwatia wote wawili hatiani kwenye makosa sita kati ya saba yaliyokuwa yakiwakabili.Hakimu Kahyoza alisema wakati akisoma hukumu hiyo kuwa, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa mashtaka, mahakama imeona kuwa pasi na shaka, washtakiwa hao wana hatia katika makosa sita kati ya saba.


Alisema upande wa mashtaka umeweza kuthitisha shtaka la kula njama kwa kuwa katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa Hussein ambayo yalipokelewa kama kielelezo na mahakama hiyo, yanaeleza kuwa alipewa maelekezo na ndugu yake Maranda kuhusu kuandaa nyaraka za kughushi jina la kampuni pamoja na mahali ambapo ofisi ya kampuni hiyo itakuwepo.

  
 “Katika ushahidi ulitolewa na Jamhuri hapa mahakamani, hakuna ubishi kama washtakiwa walighushi nyaraka za kusajili jina la kampuni kutumia majina ya Paul Tobias na Fundi Kitunga, mahakama hii inaamini shtaka hili kweli washtakiwa walighushi nyaraka hizo.”


Akielezea shitaka la kuwasilisha nyaraka bandia, Hakimu Kahyoza alisema washtakiwa waliwasilisha nyaraka hizo wakati huo (United Bank of Afrika (UBA) ambapo walifungua akaunti ya pamoja. Alisema kwa kutumia majina ya uongo (Paul na Fundi), mahakama inaamini washtakiwa walighushi hati ya kuhamisha deni wakionyesha ni wakala kutoka Kampuni ya   B.Graciel ya Ujerumani kwenda Kampuni ya Money Planers & Consultant ya Tanzania.


Hakimu huyo alisema kuwa mahakama inaamini washtakiwa waliwasilisha BoT hati za kughushi kwa ajili ya maombi ya Sh. bilioni 2.2 ambazo walifanikiwa kuhamishiwa kupitia akaunti yao iliyokuwa benki ya UBA. Aliongeza kuwa: "Mahakama inawaona washtakiwa hao hawana hatia kwenye shtaka la sita la wizi ambalo hakuna shahidi wa upande wa Jamhuri aliyethibitisha kama washtakiwa waliibia BoT.”

Aliongeza kwamba kutokana na maelezo yote hayo hakuna ubishi kwamba washtakiwa walijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu baada ya kula njama, kughushi nyaraka na kuwasilisha hati bandia BoT. Kwa upande wa Hakimu Masengi alisema katika hukumu yake ambayo itakuwa kumbukumbu ya mahakama, ameona ushahidi uliotolewa na washtakiwa hauna nguvu ya kuwatia hatiani na kwamba jukumu la kuthibitisha kesi ni la Jamhuri.

 
Alisema katika kesi hiyo, BoT haijafika mahakamani hapo kueleza au kulalamika kama waliibiwa fedha hizo na hata ile kampuni ya B.Graciel ya Ujerumani hawajalalamika kuibiwa fedha hizo na washtakiwa. Hakimu Masengi alisema Wakala wa Majina ya Biashara (Brela) hawajalalamika kupokea nyaraka zilizoghushiwa na washtakiwa mahakamani hapo na kwamba ushahidi huo wa Jamhuri unaonyesha ni jinsi gani wameshindwa kuondoa mashaka mbele ya mahakama hiyo.

Hakimu Revovat alisoma hukumu hiyo kwamba washtakiwa wataanza kutumikia kiifungo hicho kuanzia jana sambamba na kifungo cha awali. Katika kesi hiyo,washtakiwa wanadaiwa kuwa Machi 20 na Desemba 25, mwaka 2005 washitakiwa walijipatia ingizo la Sh. 2,266,049,041.25 wakidai kwamba Kampuni ya B.Graciel ya Ujerumani imehamishiwa deni na Kampuni ya Money Planers & Consultant ya Tanzania.

WAZIRI ALIYEJIUZULU KWA KUZAMA BOTI YA MV SKAGIT APONGEZWA


Mhe. Hamad Masoud Hamad

Chama cha Wananchi (CUF) kimeungana na wananchi wengine mbalimbali kumpongeza Mhe. Hamad Masoud Hamad kwa hatua yake ya kujiuzulu nafasi ya kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni siku chache tu baada ya kuzama kwa boti ya Mv Skagit na kuua mamia ya watu.


Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sera wa CUF, Salum Dimani, amesema kuwa chama chao, ambacho ndicho anachotoka Mhe. Hamad, kimebaini kuwa waziri huyo wa zamani hakufanya kosa lolote, bali amechukua hatua hiyo kwa nia ya kuwajibika kisiasa; hatua ambayo wametaka iigwe na viongozi wengine wa juu pindi matukio ya namna hiyo yanapotokea.  


Hamad alitangaza rasmi hatua yake ya kujiuzulu jana na kusema kuwa aliandika barua hiyo tangu Julai 20 (siku moja baada ya boti kuzama), lakini alitakiwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kuwa afanye subira na jana ndipo akakubaliwa.


Jana, Dk. Shein alimteua Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani (CUF), Rashid Seif Suleiman kuwa mrithi wa nafasi ya Hamad katika kuongoza wizara hiyo ya Miundombinu na Mawasiliano.

RAIS WA GHANA ATTA MILLS AFARIKI GHAFLA LEO

ALIINGIA MADARAKANI AKITOKEA UPINZANI 2009

Hayati Atta Mills enzi za uhai wake.

ACCRA, Ghana

Rais wa Ghana, John Atta Mills, aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi ya kansa ya koo, amefariki dunia katika jiji kuu la nchi hiyo, Accra.


Taarifa kutoka katika ofisi yake yake zilieleza kuwa rais huyo mwenye miaka 68 alikufa saa chache tu baada ya kuzidiwa, lakini hakukuwa na maelezo zaidi.


"Kwa huzuni kubwa... tunatangaza juu ya kifo cha ghafla na kisichotarajiwa cha rais wa Jamhuri ya Ghana," taarifa hiyo ilisema.


Atta Mills ameliongoza taifa hilo la magharibi mwa Afrika tangu mwaka 2009 wakati chama chake kilichokuwa cha upinzani kiliposhinda katika uchaguzi mkuu wan chi hiyo.


Msaidizi wa rais amesema kwamba Atta Mills alilalamika kusumbuliwa na maumivu jana jioni na akafa leo mchana, shirika la habari la Reuters liliripoti.


Alirejea Ghana baada ya kutoka Marekani alikokwenda kuchunguzwa afya yake.

MIILI MINGINE 21 YA BOTI ILIYOZAMA YA MV SKAGIT YAOPOLEWA BAHARINI LEO, SASA MAITI ZAFIKIA 98


Wananchi wakiendelea na zoezi la uopoaji maiti za ajali ya kuzama kwa Mv Skagit.
Maiti zaidi wakiteremshwa baada ya kuopolewa baharini.

Askari waliokuwa wakishughulikia zoezi la kusaka miili ya watu waliokufa katika ajali ya Mv Skagit wakiwa katika eneo la Bandari ya Zanzibar kabla zoezi hilo kusimamishwa awali. (Picha: Ramadhan Othman - Ikulu)

Miili mingine 21 ya watu waliozama na boti ya Mv Skagit iliyokuwa ikisafiri kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea Zanzibar imepatikana leo na hivyo kuongeza idadi ya maiti wote waliopatikana kufikia 98.


Taarifa zilizothibitishwa na Polisi Zanzibar jioni hii zimeeleza kuwa miili hiyo imepatikana katika maeneo mbalimbali, yakiwamo ya Chumbe kulikotokea ajali hiyo, Pume na Punguja.


Jeshi hilo limesema kuwa miongoni mwa miili iliyopatikana, umo wa mgeni mmoja kutoka Uholanzi na kwamba.

Licha ya awali kutangazwa na Serikali juu ya kusitishwa rasmi kwa zoezi la kutafuta miili zaidi, bado juhudi zimekuwa zikiendelea kufanywa na serikali kwa kushirikiana na wananchi katika kusaka miili ya watu waliokufa kutokana na ajali hiyo.


Wakati ikizama katika eneo la Chumbe, boti hiyo ilikuwa na watu zaidi ya 340. Inahofiwa kuwa baadhi ya miili ya waliokufa bado imenasia ndani ya boti hiyo ambayo imezama chini kabisa mwa kina kirefu cha bahari kinachokadiriwa kuwa ni cha zaidi ya mita 60.


Boti ya Mv Skagit ilikumbwa na ajali hiyo Julai 19 wakati ikiwa katika eneo la Chumbe. Ilidaiwa kwamba awali ilipigwa na dhoruba kali mishale ya saa 7:00 mchana, ikapinduka na kisha boti hiyo ndipo ikazama yote baharini.

NDEGE YA PRECISION YENYE ABIRIA 30 YAPASUKA TAIRI JIONI HII IKIWA NA ABIRIA 30 KIGOMAAbiria 30 wamenusurika kufa baada ya ndege ya Precision Air aina ya ATR 200, yenye namba za usajili  5HPW kupasuka tairi lake la tatu wakati ikikaribia kupaa katika Uwanja wa Ndege wa Kigoma na kuelekea jijini Dar es Salaam.

Taarifa zimeeleza kuwa tukio hilo limetokea saa 11:00 jioni na hatma ya safari ya abiria hao inasubiri maelekezo zaidi kutoka kwenye ofisi za ndege hiyo jijini Dar es Salaam.

BOCCO APIGA 'HAT-TRICK' SIMBA IKIAGA KAGAME

Wachezaji wa Azam wakimpongeza 'muuaji' wa Mnyama, John Bocco (katikati) wakati wa mechi yao ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni. Azam ilishinda 3-1.
Mwinyi Kazimoto (kushoto) na  Felix Sunzu (kulia) wa Simba wakiwania mpira dhidi  Kipre Bolou wa Azam wakati wa mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Kagame leo jioni.


Kipa wa Azam, Deogratius Munishi wa Azam (kushoto) akijiandaa kudaka mpira mbele ya straika wa Simba, Felix Sunzu wakati wa mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni. 
Winga Uhuru Selemani wa Simba (kulia) akipiga mpira mbele ya beki Ibrahim Shikanda (kushoto) huku Khamis Mcha (katikati) akijiandaa kutoa msaada wakati wa mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.

Siku ya kufa nyani.... Kiungo mpya wa Simba, Mussa Mudde akitolewa kwa machela baada ya kuuamia vibaya mguu wake wakati wa mechi yao dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa leo.

Mussa Mudde (katikati) akitoka uwanjani hukua kisaidiwa baada ya kuumia mguu katika mechi waliyolala kwa Azam leo.

Na Mwandishi Wetu
STRAIKA John Bocco 'Adebayor' alifunga magoli yote matatu na kuiwezesha timu yake ya Azam FC kutinga nusu fainali ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Simba katika mechi yao ya robo fainali kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.

Kwa ushindi huo, Azam itacheza nusu fainali dhidi ya Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambayo mapema leo mchana iliwachapa Atletico ya Burundi 2-1 huku Taddy Etikiema wa Vita akifunga goli lake la 6 la mashindano hayo mwaka huu. Etikiema anafuatiwa na Said Bahanuzi wa Yanga mwenye magoli 5 katika mbio za kuwania kiatu cha mfungaji bora.

Nusu fainali ya pili kesho itakuwa ni baina ya Yanga na APR ambazo zitakutana kwa mara ya pili ndani ya wiki moja baada ya Ijumaa wenyeji kushinda 2-0 katika mechi yao ya mwisho ya Kundi C.

Azam walitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na juhudi zao zilizaa bao la kuongoza katika dakika ya 18 kupitia kwa Bocco aliyeunganisha kwa kichwa cha mkizi mpira wa krosi ya Ibrahim Shikanda na wangeweza kwenda mapumziko wakiongoza 2-0 kama wangepewa na kufunga penalti iliyoonekana kuwa ya wazi wakati mshambuliaji wao alipoangushwa ndani ya boksi.

Bocco, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu ulioisha, aliifungia Azam bao la pili katika dakika ya 46 baada ya Uhuru Selemani kunyang'anywa mpira kirahisi na mfungaji kukimbia na mpira akitokea kulia mwa uwanja na kuingia ndani ya boksi kabla ya kupiga shuti lililomshinda kipa Juma Kaseja.

Simba walipata matumaini mapya ya kurejea mchezoni baada ya beki wa kushoto, Shomari Kapombe kufunga goli zuri la juhudi binafsi katika dakika ya 53, lakini shujaa wa Azam, Bocco, alimpeleka tena wavuni Kaseja kuokota mpira katika dakika ya 73 kwa shuti kali la nje ya 18 na kuandika bao lake la nne la michuano hii.   

Kipigo cha Simba kilihitimisha kampeni mbaya kwa mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo ambao wametwaa Kombe la Kagame mara 6, baada ya kufungwa mechi mbili (dhidi ya URA ya Uganda na Azam), sare moja (dhidi ya Vita Club) na kushinda moja tu (dhidi ya timu dhaifu ya Ports ya Djibout) kati ya nne walizocheza mwaka huu.

Baada ya mechi hiyo ambayo Azam walilipa kisasi cha kufungwa kwa penalti katika fainali ya Kombe la Urafiki wiki mbili zilizopita kwenye uwanja huo, kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic alilalamikia muda mfupi wa maandalizi.

"Tulikuwa na siku 10 tu za kujiandaa. Michuano mikubwa kama hii unahitaji mwezi wa maandalizi," alisema Mserbia huyo ambaye timu yake ilikubali kwenda Zanzibar kushiriki kombe dogo la Urafiki ambalo halikuwepo kwenye ratiba huku mahasimu wao Yanga wakikataa na kupelekea timu ya vijana ambayo nayo ilikuja kutimuliwa na waandaaji chama cha soka cha Zanzibar (ZFA).

Kocha aliyejaa furaha wa Azam, Stewart Hall, aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo akisema walifuata maelekezo yake na kuweka juhudi kubwa uwanjani na akasisitiza kwamba walistahili ushindi mnono zaidi walikuwa na nafasi nyingi za kufunga na walinyimwa penalti.

"Nawapongeza wachezaji, wamecheza vizuri leo kuliko mechi iliyopita, wamefuata maelekezo yangu, wameweka juhudi. Tulikuwa na nafasi ya kupata ushindi mkubwa zaidi kwani tulitengeneza nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza na tulinyimwa penalti, ambayo kwangu ilikuwa ni penalti," alisema Hall.

Vikosi katika mechi ya jana jioni vilikuwa; Simba: Juma Nyosso, Mussa Mude/ Salim Kinje (dk. 83), Jonas Gerard Mkude/ Amri Kiemba (dk. 81), Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi 'Boban', Felix Sunzu na Uhuru Selemani/ Kigi Makasi (dk.66).

Azam: Deogratius Munishi 'Dida', Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said Morad, Aggrey Morris, Kipre Bolou/ Ramadhani Chombo 'Redondo' (dk. 17), Kipre Tchetche/ George Odhiambo 'Blackberry', Salum Aboubakar, John Bocco 'Adebayor', Ibrahim Mwaipopo na Khamis Mcha/ Jabir Aziz (dk. 70).

KOSCIELNY AJIFUNGA MIAKA MINGI ARSENAL

Laurent Koscielny

BEKI wa kimataifa wa Ufaransa, Laurent Koscielny amesaini mkataba mpya wa muda mrefu na Arsenal, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England imetangaza leo.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 amekuwa nguzo muhimu ya ulinzi ya kikosi cha kocha Arsene Wenger na kiwango cha juu alichoonyesha katika ligi hiyo ya juu Uingereza kimempatia nafasi ya kuichezea timu yake ya taifa ya Ufaransa mara 4 ikiwemo kuitwa katika kikosi kilichoenda kwenye fainali za Euro 2012.

"Laurent amekuwa katika kiwango bora pamoja nasi kwa misimu miwili iliyopita," Wenger aliiambia tovuti ya klabu hiyo (www.arsenal.com).

"Unapozingatia hilo tangu 2009 alipokuwa akicheza katika daraja la kwanza Ufaransa (Ligue 2) na kwamba hivi sasa anacheza kwa kiwango cha juu katika Ligi Kuu ya England na timu yake ya taifa, maendeleo aliyoonyesha ni ya kipekee kabisa.

"Laurent ni mchezaji wa kiwango cha juu na nina furaha sana ameamua kujifunga kwenye klabu."

Koscielny aliisaidia Arsenal kufuzu kucheza Ligi ya Klabu Bingwa 2012/13 wakati alipofunga goli la ushindi dhidi ya West Bromwich Albion katika siku ya mwisho wa msimu.

Alisema amefurahia kuongeza mkataba huo na anatarajia makubwa ya baadaye akiwa na Gunners.

"Nina furaha kufikia muafaka na klabu. Nimekuwa na kipindi kizuri hapa na natarajia mafanikio makubwa ya baadaye na Arsenal," alisema Koscielny.

Beki huyo wa kati alijiunga na Arsenal akitokea katika klabu ya FC Lorient mwaka 2010 na baada ya majeraha kumharibia mwanzo wake, ameibuka na kucheza jumla ya mechi 85 akiwa na Arsenal.

MOURINHO ASHINDA BONGE LA TUZO URENO


Jose Mourinho akishangilia baada ya kutwaa taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wakati akiifundisha Inter Milan ya Italia.
LISBON, Ureno
KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho atapokea tuzo ya Fernando Soromenho Ijumaa ambayo hutolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Ureno (CNID) kutokana na mafanikio yake katika mchezo wa soka.

Kocha huyo mwenye miaka 49, atakabidhiwa tuzo hiyo kwenye hoteli ya Pestana Palace mjini Lisbon, na baada ya hapo atazungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Hiyo ni tuzo inayopewa heshima ya juu zaidi kutoka CNID, ambayo ilianzishwa mwaka 1967.

Mourinho, aliyeanza kazi ya ukocha mwaka 2000 katika klabu ya Benfica, aliisaidia Porto kutwaa taji moja la Kombe la UEFA na kombe jingine la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika kipindi cha miaka miwili ya kuiongoza klabu hiyo.

Akaendeleza moto wake kwa kutwaa mataji kadhaa baada ya kuhamia Chelsea na Inter Milan kabla ya kutua Real Madrid wakati wa usajili wa majira ya kiangazi mwaka 2010. Hadi sasa, tayari ameshaipa Real Madrid Kombe la Mfalme (Copa del Rey) na jubingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania.

BAHANUZI APITWA MAGOLI KAGAME

Said Bahanuzi akishangilia moja ya mabao yake dhidi ya Wau Salaam ya Sudani Kusini kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumanne Julai 17, 2012. Bahanuzi alifunga magoli mawili, Yanga ilishinda 7-1. Picha: Globalpublishers.info

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Said Bahanuzi amepitwa kwa goli moja na Taddy Etikiema wa Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo baada Etikiema kuifungia timu yake goli la kuongoza katika dakika ya 7 ya mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Kagame waliyoshinda 2-1 dhidi ya Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya Atletico ya Burundi.

Vita sasa itacheza nusu fainali dhidi ya mshindi wa mechi inayoanza hivi punde baina ya Simba na Azam FC zote za Dar es Salaam.

Taddy alifunga goli hilo akitumia makosa ya beki kujichanganya wakati akimrudishia mpira kipa wake.

Etikiema sasa amefikisha magoli 6 katika mechi nne na kumuacha Bahanuzi akiwa na magoli 5. 

Bahanuzi alifunga goli lake la tano kwa kichwa jana kufuatia krosi ya beki mpya wa kulia Juma Abdul katika dakika ya kwanza ya kipindi cha pili na kuisawazishia timu yake ya Yanga iliyoenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya mabingwa wa Zanzibar, Mafunzo. 


Goli hilo la Bahanuzi liliilazimisha mechi hiyo kuamuliwa kwa kupigiana penalti baada ya dakika dakika 90 kumalizika matokeo yakiwa 1-1. Yanga walishinda kwa penalti 5-3 na kutinga nusu fainali ambapo sasa watawakabili APR ya Rwanda keshokutwa.


Vikosi katika mechi inayotarajiwa kuanza punde ni; Simba: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Shomari Kapombe, Lino Masombo, Juma Nyosso, Mussa Mude, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi 'Boban', Felix Sunzu na Uhuru Selemani.

Azam: Deogratius Munishi 'Dida', Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said Morad, Aggrey Morris, Kipre Bolou, Kipre Tchetche, Salum Aboubakar, John Bocco 'Adebayor', Ibrahim Mwaipopo na Khamis Mcha.  MASHINDANO YA DANSI MIA MIA YAINGIA NUSU FAINALI


Wasanii wa kikundi kudansi cha The Chocolote wakionyesha mbwembwe zao wakati wa mashindano ya 100% yanayoandaliwa na televisheni Na.1 kwa vijana Afrika Mashariki ya EATV. Washindi wataondoka na zawadi ya Sh. milioni 5.     

Kikundi pekee cha akina dada kwenye mashindano ya Dance 100% wakionyesha vitu vyao kwenye robo fainali. Mashindano haya yameandaliwa na EATV.        

Sehemu ya umati wa mashabiki waliofurika kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam kushuhudia mashindano ya Dansi Mia Mia.
Watasha wakifuatilia staili za hatari za kudansi kutoka kwa vijana wa Kitanzania kwenye viwanja wa Leaders Club Kinondoni...

Vijana wakionyesha mambo...

Madansa wa kikundi cha Best Friends wakifanya mabalaa yao wakati wa mashindano ya Dance Mia Mia...

Dansa wa kikundi cha Best Friends akizungukia kichwa wakati wa mashindano ya Dance Mia Mia...

Madansa wa kikundi cha Best Friends wakifanya mabalaa yao wakati wa mashindano ya Dance Mia Mia...

Madansa wa kikundi cha T-Africa wakionyesha staili zao wakati wa mashindano ya Dance Mia Mia...

WABUNGE WALIA NA MATUSI YA AKINA ‘KANGA MOJA NDEMBENDEMBE’, ‘KANGA MOKO LAKI SI PESA’ NA ‘KITU T’

Astaghafirullahi.... hii sasa noma. Uchezaji huu wa mnenguaji mmojawapo wa akina 'Kanga Moko' nd'o uliomchefua mbunge hadi akalalamika bungeni leo.
Mmmhhh... uchezaji gani huu jamani? Ndo mambo ya akina 'Khanga Moko Laki Si Pesa, Milioni Moja Paketi Money'
Tobaaa....! Namna hii tutasalimika kweli? Huyu naye ni memba wa walewale akina 'Kitu T' na 'Kanga Moko'
Uuuuwwwiiiii.....mwenzenu nafwa na kiuno hiki... haki ya nani siangalii tena!

Mtazame na huyu... nd'o walewale. Tatizo ni hiyo khanga yenyewe moja, ambayo unaambiwa imeloweshwa kidogo na kuwa ndembendembe! Kwanini wabunge wasihofie upotofu wa maadili?

Ohooo....! Hawa nao wamevaa vizuri katikati ya mwili, lakini chini ni khanga moja ndembendembe na bado wanajibinua kihasara hasara. Ni balaaa tupu!
Apo chachaaaa....! Huu wote ni uchokozi wa akina Khanga Moko  

Mama weeee.....! Hii si mitego jamani?

Wabunge wa viti maalum, Mhe. Tawhida wa Zanzibar na Mhe. Dk. Getrude Rwakatare wameitaka serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti vitendo vya uvaaji wa hovyo na unaokiuka maadili wa makundi ya unenguaji kama ya ‘Kanga Moja Ndembendembe Laki Si Pesa’.

Wabunge hao wameyasema hayo bungeni mjini Dodoma mchana huu wakati wakichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Awali, Mhe. Tawhida  alisema kwamba vivazi hivyo vya makundi kama ‘Khanga Moja Laki Si Pesa’ vinadhalilisha wanawake kwani wanenguaji wake huvaa khanga moja nyepesi inayoonyesha sehemu kubwa ya miili yao na pia uchezaji wao hujaa matusi ambayo hayapaswi kuachwa hivi hivi.

Wakati akielezea kilio chake kuhusiana na vikundi vya aina ya Khanga Moko, Mhe. Mchungaji Rwakatare alienda mbali zaidi kwa kufafanua kuwa wanenguaji hao (akina Khanga Moko) hulowesha khanga zao na kucheza kwa namna ambayo inakwenda kinyume na maadili.

Akaitaka serikali kuingilia kati na kuchukua hatua za kukomesha vikundi vya aina hiyo vinavyochangia sana katika kuharibu maadili.

SUGU ATAKA MIKATABA BORA YA AJIRA KWA KINA JULIO, MKWASA

Mhe. Sugu akifanya vitu vyake bungeni

Kocha Jamhuri Kihwelu 'Julio' akiwajibika wakati akiifundisha timu ya taifa ya vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 23.
Kocha Charles Boniface Mkwasa akiwa kibaruani wakati akiiongoza timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.
 Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Mhe. Joseph Mbilinyi ‘Mr. II-Sugu’ ameitaka serikali itekeleze mara moja ahadi yake ya kuhakikisha kwamba makocha wazawa wanaandaliwa mikataba yao ya ajira ili nao walipwe vizuri na kwa uhakika tofauti na ilivyo sasa ambapo wageni pekee ndio hufaidika kwa kulipwa mamilioni ya pesa.

Mhe. Sugu ameyasema hayo mchana huu wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mwaka ujao wa fedha.

Sugu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa wizara hiyo, alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa makocha wazawa (kama Jamhuri Kihwelu ‘Julio’,  Boniface Mkwasa, Juma Pondamali) wakikosa mikataba itakayowahakikishia maslahi bora huku wageni wamekuwa wakilipwa fedha nyingi; ambapo hata katika bajeti ya sasa, imeonyesha kuwa zimetengwa jumla ya Sh. milioni 400 kwa ajili tu ya kuwalipa mishahara makocha wa kigeni.

Alikumbushia kuwa katika bajeti iliyopita, aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliahidi kutekeleza ushauri wa kambi ya upinzani kuhusiana na suala hilo na kwamba, tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeanza mchakato wa kuandaa mikataba ya makocha wazawa.

“Je, utekelezaji wa suala hili umefikia wapi?” alihoji Sugu.

PUYOL AREJEA BAADA YA KUPASULIWA GOTI

Carles Puyol

BARCELONA, Hispania
BEKI wa Barcelona, Carles Puyol amerejea mazoezini kwa mara ya kwanza tangu alipofanyiwa upasuaji wa goti mwezi Mei, klabu hiyo ya La Liga ilisema jana.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania mwenye umri wa miaka 34 alifanyiwa upasuaji wa goti na akakaa nje katika wiki kadhaa za mwisho wa msimu, jambo lililomfanya akose ubingwa wa taifa lake wa Euro 2012 nchini Poland na Ukraine.

"Nahodha alifanya mazoezi mbali na wachezaji wenzake kabla hawajasafiri kwenda Ujerumani leo kwa ajili ya mechi yao ya kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Hamburg," Barca ilisema katika tovuti yao (www.fcbarcelona.com).

"Puyol atafanyiwa uchunguzi mwingine wa kiafya Jumatatu ijayo, Julai 30, kuthibitisha uzima wake ili arejee kikamilifu mazoezini na wenzake - siku ambayo wachezaji wa kimataifa wa Hispania wataanza mazoezi," taarifa hiyo ilisema.

Mchezaji mwenzake Puyol, Dani Alves aliongeza katika mkutano na waandishi wa habari: "Nina furaha sana kwamba Puyi amerejea, kwamba yuko katika hali nzuri na anapona.

"Nadhani ukiwa na Puyi huhitaji kuangalia umri wake, kwa sababu haumaanishi chochote. Kwangu mimi, yeye ni kama mtoto wa miaka miwili."

SEEDORF AANZA NA KIPIGO BOTAFOGO

Mchezaji wa soka wa Uholanzi, Clarence Seedorf (kulia) akionyesha fulana iliyoandikwa "Seedorf, Carioca wa ukweli kuliko Waholanzi wote" huku Meya wa Rio de Janeiro, Eduardo Paes, akionyesha jezi ya Botafogo kabla ya mkutano wake wa kwanza na vyombo vya habari katika klabu yake mpya ya Botafogo katika jumba la Cidade Palace mjini Rio de Janeiro, Brazil Julai 9, 2012. Klabu ya Botafogo imemsajili Seedorf (36) kwa mkataba wa miaka miwili. Picha: REUTERS

KIUNGO wa zamani wa AC Milan, Inter Milan, Real Madrid na Ajax Amsterdam, Clarence Seedorf ameanza kucheza ligi kuu ya Brazil na kipigo baada ya klabu yake mpya Botafogo kulala 1-0 nyumbani dhidi ya Gremio.

Mholanzi huyo mwenye umri wa miaka 36, ambaye ameelezwa na rais wa Botafogo, Mauricio Assuncao kama mchezaji wa kigeni gwiji zaidi kupata kusajiliwa na timu hiyo ya Brazil, alicheza kwa kiwango cha chini, ingawa alipigiwa makofi na mashabiki wa nyumbani wakati akipumzishwa kuelekea mwishoni mwa mechi hiyo.

"Hali ya hewa ni nzuri, natumai kila mechi itakuwa hivi," aliwaambia waandishi wa habari baada ya mechi hiyo ya Jumapili.

"Seedorf amekuwa pamoja nasi kwa wiki mbili tu," alisema kocha Oswaldo de Oliveira. "Yeye ndio anaanza msimu wakati sisi tuko katikati."

Botafogo ni wa nane katika ligi hiyo yenye timu 20 kwa kuwa na pointi 17 kutokana na mechi 11.

TIM CAHILL AJIUNGA NA THIERRY HENRY

Tim Cahill

EVERTON imeafikiana bei na klabu ya New York Red Bulls kwa ajili ya uhamisho wa kiungo wa Australia, Tim Cahill kwenda kwenye timu hiyo ya Ligi Kuu ya Marekani anayoichezea mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Thierry Henry.

"Tim atahamia Red Bulls kwa ada iliyofichwa, kutegemea maafikiano binafsi ya mchezaji na kama atafuzu vipimo vya afya. Atasafiri kwenda Marekani katika siku chache zijazo," Everton ilisema katika tovuti yao (www.evertonfc.com).

Vyombo vya habari wa Uingereza vimeripoti kuwa ada ya uhamisho huo ni  dola milioni 1.55.

Kiungo huyo wa ushambuliaji mwenye umri wa miaka 32 alifunga magoli 68 katika mechi 278 alizoichezea Everton baada ya kujiunga na klabu hiyo akitokea Millwall mwaka 2004.

Pia amefunga magoli 24 katika mechi 55 za timu yake ya taifa ya Australia na amecheza fainali mbili za Kombe la Dunia nchini Ujerumani na Afrika Kusini.