Saturday, November 24, 2012

HARRY REDKNAPP ATHIBITISHA YEYE NDIYE KOCHA MPYA WA QPR... ATAANZA KAZI LEO JIONI KWA KUIONGOZA KATIKA MECHI YAO DHIDI YA MANCHESTER UNITED... ANA KAZI KUBWA KUINASUA MKIANI MWA MSIMAMO WA LIGI KUU

Harry Redknapp
LONDON, England
Kocha wa zamani wa Tottenham, Harry Redknapp amethibitisha kuwa yeye ndiye kocha mpya wa QPR na ataanza kazi leo jioni kwa kuiongoza kutokea jukwaani timu yake hiyo mpya itakayocheza ugenini kusaka ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu ya England msimu huu kwa kucheza dhidi ya vinara Manchester United.

Ingawa hadi kufikia wakati wa mechi hatakuwa amekamilisha taratibu za uhamisho na kuwapo katika benchi rasmi la ufundi, Redknapp ameiambia Sky Sport kwamba tayari amemalizana na QPR na kwamba, anachosubiri ni kwenda kwenye Uwanja wa Old Trafford kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya Man U kutokea jukwaani.

Kocha huyo mwenye miaka 65, hakutaka kueleza kiundani kuhusiana na makubaliaono waliyofikia na uongozi wa QPR.

"Mnapaswa kusubiri na kuona," amesema Redknapp.

Redknapp amekuwa bila timu kwa miezi mitano sasa baada ya kutimuliwa na Tottenham tangu Juni.

Atalazimika kufanya kazi ya ziada kuinasua QPR kutoka mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England kwani licha ya timu hiyo kufanya usajili 'bab'kubwa' uliowajumuisha nyota kadhaa wakiwamo kipa Mbrazili Julio Cesar,  beki Jose Bosingwa kutoka Chelsea na kiungo Esteban Granero kutoka Real Madrid, bado timu hiyo imekuwa na matokeo mabovu mno na hadi sasa haijawahi kushinda katika mechi zote 12 walizocheza katika ligi hiyo msimu huu.

No comments:

Post a Comment