Wednesday, September 5, 2012

MAN UTD YAMSAJILI STRAIKA WA CHILE HENRIQUEZ

Fergie akiwa na Henriquez baada ya kukamilisha usajili wa straika huyo mwenye umri wa miaka 18


LONDON, Uingereza
STRAIKA wa timu ya taifa ya Chile ya vijana wa umri chini ya miaka 23, Angelo Henriquez amekamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Manchester United, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England imetangaza leo kwenye tovuti yao.

Henriquez (18) amejiunga akitokea katika klabu ya Universidad de Chile kwa ada ya uhamisho ambayo haitajwi. Vyombo vya habari vya Uingereza vimesema kuwa mchezaji huyo amefuzu vipimo vya afya na na alipata kibali cha kufanya kazi tangu mwezi uliopita.

"Angelo ameonyesha kiwango kikubwa katika muda mfupi aliokaa hapa," kocha wa United, Alex Ferguson aliiambia manutd.com.

"Kasi yake ni 'aseti' na anausoma mchezo haraka sana kulingana na umri wake mdogo.

"Tuna rekodi ya kujivunia ya kuendeleza vipaji vidogo, na Angelo anafiti katika sifa ya mchezaji wa United - ana kipaji, anashambulia na ni mtu ambaye anacheza soka tamu."

Pia aliliambia jarida la Inside United: "Tulimfuatilia wakati akiwa na umri wa miaka 14. Alipotimiza miaka 18, tungeweza kumchukua; ni kwa mara ya kwanza sasa tunaweza kusajili wachezaji nchini humu, wakiwa na miaka 18."

Henriquez alisema: "Manchester United ni timu kubwa na ina kocha baab'kubwa. Kuwa sehemu ya klabu hii ni heshima kubwa, nashindwa kusubiri kuanza kuitumikia."

No comments:

Post a Comment