Tuesday, July 17, 2012

YANGA YAWAFUTA MACHOZI MASHABIKI KWA 7-1

Hamis Kiiza 'Diego' (katikati) wa Yanga akishangilia goli lake pamoja na wachezaji wenzake Stephano Mwasika (kushoto) na Said Bahanuzi (kulia) wakati wa mechi yao ya Kundi C la michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.
Gooooooo! Said Bahanuzi akishangilia goli lake baada ya kufunga dhidi ya Wau Salaam wa Sudan Kusini wakati wa mechi yao ya Kundi C la michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.

Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) wamewafuta machozi mashabiki wao kwa ushindi mnono wa 7-1 dhidi ya timu dhaifu ya Wau Salaam ya Sudan Kusini katika mechi yao ya pili ya Kundi C ambayo kocha wao Mbelgiji Tom Saintfiet alisema walipaswa kushinda 10-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.

Mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza 'Diego' alifunga 'hat-trick', Said Bahanuzi aliyetua Jangwani katika kipindi hiki cha usajili akitokea Mtibwa Sugar alifunga mawili na Nizar Khalfan na Stephano Mwasika kila mmoja aliongeza moja, katika mechi ya upande mmoja ambayo nafasi walizokosa Yanga zilikuwa ni nyingi kuliko walizofunga.

Hata hivyo, kipindi cha kwanza washambuliaji wa Yanga walionyesha umakini mkubwa katika umaliziaji kwani kati ya jumla mashuti 8 waliyopiga, 6 yalitinga wavuni.

Kukosa nafasi mfululizo kulionekana kumkera kocha Tom, ambaye alikuwa hatulii katika nafasi yake na alipohojiwa baada ya mechi alikiri kutofurahishwa na jambo hilo.

"Nilitaka tuweke rekodi kwa kufunga magoli 10 kwani tulitaka kuwapa kitu tofauti mashabiki ambao wamekuwa wakiisapoti timu. Unapopata nafasi ni vyema ukazitumia kwa sababu unapocheza dhidi ya timu ngumu si rahisi kupata nafasi za kuchezea. Na mwisho tukafanya makosa tukaruhusu goli, hupaswi kufanya makosa kama yale," alisema Saintfiet.

"Hata hivyo nina furaha. Kushinda 7-1 si jambo dogo, ila tutaangalia tusifanye makosa katika siku zijazo."

Aidha, kocha Tom alisema anapenda kuona timu yake inamaliza katika nafasi ambayo itawafanya wasicheze katika hatua inayofuata dhidi ya timu za Simba, URA na Azam, ambazo alisema ni timu ngumu.

Ushindi huo umeibakisha Yanga katika nafasi ya tatu ya msimamo ya kundi lao ikiwa na pointi 3, moja nyuma ya vinara APR ya Rwanda yenye pointi 4 na Atletico ya Burundi iliyo na pointi 4 pia katika nafasi ya pili baada ya timu hizo mbili kutoka sare ya 0-0 katika mechi iliyochezwa mapema saa 8:00 mchana jana.

Michuano hiyo inaendelea leo wakati mabingwa wa Tanzania Bara, Simba watakapowakabili vibonde wa Kundi A, Ports ya Djibout, ambayo nayo ilianza kwa kuchapwa 7-0 na Vita Club ya DRC Jumapili. Simba ililala 2-0 dhidi ya URA katika mechi yao ya kwanza. Vita itacheza dhidi ya URA katika mechi ya mapema leo mchana.

Kikosi cha Yanga katika mechi ya leo kilikuwa: Yaw Berko, Godfrey Taita, Oscar Joshua, Nurdin Bakari, Kelvin Yondani/ Idrissa Rashid (dk. 46), Athumani Idd 'Chuji', Nizar Khalfani, Haruna Niyonzima/ Rashid Gumbo (dk. 53), Stephano Mwasika/ Juma Seif 'Kijiko' (dk. 46), Said Bahanuzi na Hamis Kiiza.
 

No comments:

Post a Comment