Sunday, July 1, 2012

WANYONGE WA YANGA, WAWAKABA SIMBA


KIKOSI kilichosheheni nyota wapya na yosso waliosajiliwa hivi karibuni cha ‘Wekundu wa Msimbazi’, Simba kilikosa makali mbele ya lango na kujikuta kikishikiliwa na Express ya Uganda kwa sare ya 0-0 katika mechi yao ya kujipima nguvu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Simba ambao wiki iliyopita walishindwa pia kutambiana na Express katika mechi yao waliyocheza mjini Shinyanga na kutoka sare ya 1-1, walionyesha kandanda safi tangu mwanzo wa mechi na kutawala kwa gonga zao safi katika muda mwingi wa mchezo.
Kiungo Mussa Mudde aliyetua kwa ‘Wanamsimbazi’ akitokea katika klabu ya Sofapaka ya Kenya alikaribia kuifungia Simba bao la mapema katika dakika ya pili tu baada ya kukaribia lango na kupiga shuti ambalo hata hivyo lilidakwa na kipa Didi Mohamed wa Express.
Katika dakika ya tisa, Mudde alikaribia tena kufunga baada ya kupata nafasi nzuri lakini shuti lake likatoka nje ya lango.
Simba waliendelea kuonana na kukosa bao jingine katika dakika ya 23 kufuatia gonga safi za Uhuru Selemani na Christopher Edward kumaliziwa vibaya na Shomari Kapombe aliyepiga shuti lililopaa.   
Wageni walipoteza pia nafasi nzuri ya kufunga katika dakika ya 30 baada ya mshambuliaji Jingo Slyman kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa William Mweta wa Simba. Timu zote zilishambuliana kwa zamu katika kipindi cha pili na kukosa nafasi kadhaa za kufunga, hasa Simba ambao mara kadhaa walilikaribia lango la Express lakini mashuti ya yosso wao hayakuwa na madhara.
Simba wataondoka leo kuelekea Zanzibar kushiriki mashindano ya Kombe la Urafiki ambapo watashuka dimbani leo usiku kucheza dhidi ya Mafunzo ambapo mahasimu wao Yanga watakwenda pia Zanzibar kushiriki mashindano hayo kujiandaa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) itakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Julai 14.


No comments:

Post a Comment