Monday, July 2, 2012

VITALI KLITSCHKO: NIKISHINDA UBUNGE NAACHA NGUMI

Vitali Klitschko

BERLIN, Ujerumani
BONDIA mwenye 'mwili jumba', Vitali Klitschko anayeshikilia ubingwa wa Dunia wa uzito wa juu atatetea taji lake la WBC Sept. 8 mjini Moscow kwa kupambana na bondia asiye na umaarufu, Mjerumani Manuel Charr (27) katika kile kinachoonekana kuwa ni pambano lake la mwisho katika mchezo wa ngumi.

Mkali huyo mwenye miaka 40, ambaye mdogo wake Vladimir anashikilia mikanda ya IBF, IBO, WBA na WBO, alisema kwamba ataelekeza nguvu zake katika harakati za kuwania ubunge kwenye uchaguzi wa nchini kwao Ukraine na akichaguliwa itakuwa ndio mwisho wake wa kupigana katika ngumi.

"Kutegemeana na matokeo ya uchaguzi (Oktoba), nitaamua juu ya hatma yangu katika mchezo wa ngumi," alisema Klitschko katika taarifa yake leo.

"Kuwa mbunge na wakati huohuo kuwa bingwa wa uzito wa juu duniani haviendani."
Klitschko ameshinda mapambano 44 kati ya 46 tangu ajiunge katika ngumi za kulipwa na pambano lake la mwisho alishinda kwa pointi Februari dhidi ya bondia wa England, Dereck Chisora.

Alisema mwezi Machi kwamba pambano lake la mwisho litakuwa dhidi ya bingwa wa WBA, David Haye, ambaye alistaafu Oktoba baada ya kupoteza taji lake kwa Vladimir mwezi Julai mwaka 2011.

"Charr ni kijana, mwenye njaa ya mafanikio na pia hajawahi kushindwa," alisema Klitschko. "Hamuogopi yeyote na mara zote huangalia mbele tu. Atakuwa mkali zaidi dhidi yangu na kamwe sitafanya kosa la kumdharau."

Charr ambaye ni mzaliwa wa Syria, ameshinda mapambano yake yote 21 tangu alipojitosa katika ngumi za kulipwa mwaka 2005.

No comments:

Post a Comment