Monday, July 9, 2012

VALDES: SIJAONA MKALI BARCELONA KAMA RONALDINHO

Utampenda tu...! Ronaldinho akionyesha moja ya 'manjonjo' yake anapokuwa na mpira.
BARCELONA, Hispania
KIPA wa Barcelona, Victor Valdes amemwagia sifa Ronaldinho, akimuelezea Mbrazil huyo kuwa ndiye mchezaji mwenye "kipaji kikali zaidi" aliyepata kumuona maishani mwake.

Straika huyo mwenye miaka 32, ambaye hivi sasa anaichezea Atletico Mineiro ya Brazil, alisajiliwa Barca mwaka 2003 na kuisaidia klabu hiyo kutwaa mataji mawili ya La Liga na moja la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, kabla ya kushinda mara mbili Tuzo ya FIFA ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia na pia akatwaa mara moja Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Ulaya (Ballon d'Or)

Lionel Messi amekuwa akielezewa mara kadhaa kuwa ndiye mchezaji mkali kuwahi kutokea katika kizazi cha sasa na pia ni mmoja wa wakali wa namna ya pekee katika historia ya mchezo wa soka, lakini Valdes anaonekana kuamini kwamba Ronaldinho ndiye mkali zaidi kuliko Muargentina Messi.

"Siku zote nimekuwa nikisema kwamba 'Rony' alibadili historia ya klabu wakati akiichezea Barca," alisema katika mahojiano yake na Terra TV.

"Alikuwa kiongozi wa timu iliyobadili historia yetu.
"Hatukuwa tumetwaa kombe lolote kwa miaka mingi. Alifika na kuipa nguvu Barcelona kabla ya kuifanya ijulikane dunia nzima. Na hilo peke yake ni sababu ya kumshukuru. Naweza kusema ndio mchezaji mwenye kipaji zaidi niliyepata kumshuhudia ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo. Siku zote alikuwa akifanya vitu vipya."

Ronaldinho, aliyeihama Barca mwaka 2008 na kutimkia AC Milan, amesaini mkataba wa kuichezea Atletico Mineiro mwezi uliopita baada ya kusitisha mkataba wake na klabu ya Flamengo kufuatia mzozo kuhusiana na mshahara wake.

No comments:

Post a Comment