Wednesday, July 18, 2012

TIMU YA OKWI AUSTRIA YAANZA VIBAYA KLABU BINGWA ULAYA


Straika Emmanuel Okwi
BERNE, Uswisi
KLABU ya Salzburg ya Austria ambayo mchezaji wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi amedaiwa kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa imeanza vibaya kampeni zake za kuwania taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kupata kipigo cha ugenini cha bao 1-0 kutoka kwa FC Dudelange ya Luxemburg katika mechi yao ya hatua ya mchujo ya michuano hiyo jana.

Salzburg ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Austria (Bundesliga), hawajawahi kufikia hatua ya makundi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya tangu walipotwaliwa na Red Bulls mwaka 2005, licha ya wamiliki hao wapya kumwaga fedha nyingi za kuiendeshea timu hiyo.

Aurelien Joachim alifunga bao pekee lililowaliza Salzburg baada ya kupiga shuti kali kutoka umbali wa mita 25 zikiwa zimebaki dakika 15 kabla ya kumalizika kwa muda wa kawaida. Mtokea benchi Jonathan Soriano wa Salzburg alitolewa nje kwa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 90.

Hivi karibuni, Okwi alidaiwa kwenda Salzburg ambako atafanyiwa majaribio ya kuichezea klabu hiyo. Taarifa zaidi kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa klabu yake ya Simba, Godfrey Nyange ‘Kaburu’, zilieleza kuwa akishindwa kuishawishi Salzburg, Okwi atakwenda kujaribiwa na timu za Italia.

Imedaiwa vilevile kuwa Okwi ambaye pia ni mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, amezivutia klabu za Orlando Pirates na Mamelodi Sundows zinazoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Mbali na Salzburg ya Okwi, matokeo ya baadhi ya mechi zilizochezwa juzi za hatua ya mchujo ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ni pamoja na ushindi wa 4-1 walioupata mabingwa wa Serbia, Partizan Belgrade dhidi ya FC Valletta na Liberec ya Czech ikashinda nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Shakhtar Donetsk ya Ukraine.

No comments:

Post a Comment