Wednesday, July 11, 2012

TIKETI ZA BAYERN UWANJA WA NYUMBANI ZAMALIZIKA

* Bayern yatarajia mashabiki milioni 1.1 katika mechi zao za nyumbani za Bundesliga

*Kila tiketi ya uwanja wa Allianz Arena unaochukua mashabiki 69,000 imeshauzwa


Uwanja wa Bayern Munich wa Allianz Arena ambao kwa wakati mmoja unabeba mashabiki 69,000.

BERLIN, Ujerumani
BAYERN Munich hawajatwaa ubingwa wowote katika misimu miwili iliyopita lakini jambo hilo halijawazuia mashabiki wao kununua tiketi zote za mechi zote 17 za nyumbani za Ligi Kuu ya Bundesliga ambayo itaanza ndani ya wiki sita. 

Bayern imesema leo kwamba imeuza tiketi zote za mechi za nyumbani za msimu unaokuja katika uwanja wao wa Allianz Arena unaobeba mashabiki 69,000 kwa wakati mmoja, mauzo ambayo yanajumuisha tiketi 40,000 za msimu, na wanatarajia kupata jumla ya mashabiki wanaozidi milioni 1.1 katika mechi zao za nyumbani. 

Ligi ya Bundesliga ndiyo yenye wastani mkubwa zaidi wa mahudhurio ya watu kwa mechi duniani ambapo ni zaidi ya mashabiki 42,000.

Bayern, ambao walifungwa na Chelsea katika fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mwezi Mei, pia imesema tiketi za msimu ziliuzwa 39,500. 

"Nataka kuwashukuru mashabiki kwa jambo hili kubwa," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge leo. 

"Hii inathibitisha jinsi Bayern ilivyo na mvuto na inavyokubalika."

Bayern, ambayo pia iliangushwa katika mbio za ubingwa wa ligi kuu na kufungwa katika fainali ya Kombe la Ujerumani dhidi ya Borussia Dortmund msimu uliopita, inajivunia kutengeneza faida kwa miaka 19 mfululizo sasa.

Klabu hiyo ilitangaza faida ya euro milioni 1.3 katika msimu wa 2010/2011 kufuatia mapato ya jumla ya euro milioni 290.9 ukilinganisha na mapato ya euro milioni  312 katika msimu wa 2009/2010, na ongezeko kubwa la mauzo ya jezi kwa zaidi ya asilimia 10 kufikia euro milioni 43.9, kutoka uero milioni 38.9.

Bayern pia wanatarajiwa kupata faida ya euro milioni 20 taslimu kwa kila mwaka mara watakapomaliza kulipa deni la ujenzi wa uwanja wao mwaka 2020. 

No comments:

Post a Comment