Wednesday, July 4, 2012

TANZANIA YAPANDA NAFASI 12 VIWANGO VYA FIFA

Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Kim Poulsen (kushoto) akimuelekeza jambo John Bocco wakati wa mazoezi ya timu hiyo

Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imepanda kwa nafasi 12 katika orodha ya viwango vya ubora wa soka duniani vilivyotolewa jana na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) baada ya kushika nafasi ya 127 kutoka ya 139 ya mwezi uliopita.

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ilishinda 2-1 dhidi ya Gambia katika mechi yao ya Kundi C la kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia 2014 kabla ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Msumbiji katika mechi yao kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika. Hata hivyo, Tanzania ilitolewa kwa penalti katika mechi hiyo ya marudiano baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2.

Uganda imeendelea kuongoza ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kutokana na kushika nafasi ya 85 duniani na ya 20 kwa Bara la Afrika.

Kenya na Rwanda zimeendelea kuipita pia Tanzania baada ya zote kushika nafasi ya 125 huku kwa Afrika zikishika nafasi ya 37.

Nchi nyingine zilizo na ukanda zilizo juu ya Tanzania ni Sudan (105), Ethiopia (119) huku Burundi inayokamata nafasi ya 136 ikiwa ni miongoni mwa nchi zinazopitwa na Tanzania, nyingine zikiwa ni Somalia, Djibout na Eritrea.

Ivory Coast inayoshika nafasi ya 16 duniani bado inaongoza Afrika, ikifuatiwa na Ghana, Algeria, Libya, Mali, Zambia, Misri, Tunisia, Gabon na Nigeria.

Mabingwa wa Dunia na Ulaya, Hispania wanaoendelea kuongoza wakifuatiwa na Ujerumani, Uruguay, England, Ureno, Italia, Argentina, Uholanzi, Croatia na Denmark.

No comments:

Post a Comment