Tuesday, July 17, 2012

SUGU ADAI, ETI KAMANDA KOVA ARUDI TENA STUDIO KUANDAA UPYA FILAMU YAKE/MCHUNGAJI KUHUSU WALIOMTEKA DK. ULIMBOKA


Mhe. Sugu

Kamanda Kova
Mchungaji Gwejima
Dk. Ulimboka akiwa hospitali
Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mhe. Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr II ‘Sugu’, ametoa mpya kwa kudai kwamba taarifa aliyoitoa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuhusiana na wanaodaiwa kumteka kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka ni sawa na filamu isiyoeleweka kwa wananchi na hivyo ikaandaliwe upya.
   
Akizungumza bungeni jioni hii wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Mhe. Sugu alisema kuwa taarifa alizotoa Kova akidai kwamba kuna mtu (Mkenya Joshua Mhindi) alikwenda kuungama kwa mchungaji, ni filamu ambayo haijaeleweka kwa wananchi na kwamba, anamshauri Kamanda Kova arudi tena studio ili kuiandaa upya.

“Ni filamu ambayo haijaeleweka kwa wananchi… hivyo warudi tena studio,” alisema Sugu kabla Spika wa Bunge, Mhe. Anna Makinda kuingilia kati na kumtaka mbunge huyo akae chini kwani dakika zake za kuchangia hoja ya wizara hiyo zilikuwa zimeshamalizika.

Hivi karibuni, Kamanda Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa polisi wamemkamata raia wa Kenya, Joshua Mhindi (31) baada ya mtu huyo kwenda Kawe, katika Kanisa la Ufufuo na Uzima la Mchungaji Josephat Gwejima na kwa nia ya kuungama kwamba alihusika kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka huku akiwa na wenzake wa kikundi cha Gun Stars.

Hata hivyo, wakati wa ibada ya juzi Jumapili, Mchungaji Gwejima alikanusha baadhi ya maelezo yaliyotolewa na Kamanda Kova, ikiwemo madai kuwa Mkenya huyo alikwenda kuungama kwenye kanisa lao, huku pia akielezea hofu yake kuwa huenda mtu huyo (Mhindi) alitumwa au anasumbuliwa na matatizo ya akili.

Kwa mara nyingine, Kamanda Kova aligusia suala hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusema kuwa hayuko tayari kumjibu Mchungaji Gwejima kwavile suala hilo limeshafikishwa kortini na hivyo kulizungumzia nje ya utaratibu wa chombo hicho ni sawa na kuingilia uhuru wa mahakama.

Dk. Ulimboka alikuwa mstari wa mbele wakati wa mgomo wa madaktari uliofanyika nchini hivi karibuni kabla hajakumbwa na kadhia ya kutekwa na watu wasiojulikana ambao walimteka na kumtesa vibaya kabla ya kumtupa katika msitu wa Mabwepande jijini Dar es Salaam. Hivi sasa Dk. Ulimboka anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini.

TAHADHARI YA SUGU
Awali, katika mchango wake huo, Mhe. Sugu aliitaka Serikali kuweka hadharani matokeo ya uchunguzi wa tume iliyoundwa baada ya vurugu za wamachinga zilizotokea Novemba 11 ambapo watu kadhaa walipigwa risasi za moto na wengine kupata ulemavu, akiwemo mtu mmoja ambaye alidai kuwa hivi sasa ana hali mbaya na anasubiri kuwekewa nyonga ya bandia.

Alisema kuwa watu wa jimboni kwake (Mbeya Mjini) hawatakuwa tayari kumpokea kiongozi yeyote wa serikali ikiwa uchunguzi wa tume hiyo haujawekwa wazi.

Mhe. Sugu pia aliwatahadharisha watu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, akiwataka wawe makini katika kazi zao na kuhakikisha kuwa wanatanguliza weledi na kamwe wasikubali kutumiwa.

Alisema kuwa wizara hiyo ni nyeti katika nchi yoyote ile, na kwamba historia inaonyesha kuwa wale wanaokwenda na maji na watawala huwa ni watu wa namna yao na wala si wanajeshi, huku akitaja mfano wa yaliyotokea Misri, Algeria na Iraq.

No comments:

Post a Comment