Friday, July 13, 2012

SIMBA VUVUZELA WAANDAA HARAMBEE KUISAIDIA SIMBA QUEENS

Na Mwandishi Wetu
TAWI la klabu ya Simba la Vuvuzela la jijini Dar es Salaam limeandaa sherehe kubwa Jumapili itakayohusisha wanachama, wapenzi wa klabu hiyo pamoja na wadau mbalimbali wa soka kwenye ukumbi wa Kuala Lumpar ulioko Sinza kwa Remmy jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa tawi hilo, Paulo Makoye, sherehe hiyo ni maalum kwa ajili ya kuchangisha fedha za kuisaidia timu ya soka ya wanawake ya klabu hiyo ‘Simba Queens’ inayoshiriki ligi ya soka wanawake mkoa wa Dar es Salaam. Ligi ya mkoa wa Dar es Salaam ndiyo ligi kubwa kwa upande wa soka ya wanawake nchini.

Alisema viongozi wakuu wa klabu ya Simba pamoja na wadau mbalimbali maarufu wanatarajiwa kuhudhuria sherehe hiyo inayotarajiwa kuwa ya aina yake kutokana na maandalizi yake. Wengine ni wawakilishi wa matawi yote ya Simba jijini na mikoani, vyama vya soka vya wilaya, mkoa na taifa.

“Timu ya Simba Queens pamoja na kuwa inamilikiwa na makao makuu ya klabu ya Simba, lakini imezaliwa ikiwa chini ya tawi letu hivyo kiutendaji bado mchango mkubwa imekuwa ikipata kutoka kwetu hivyo tumeona tufanye ‘fund rising’ ili kuiwezesha timu yetu kuwa na kipato kitakachoiwezesha kushiriki vema ligi ya wanawake na hatimaye kutwaa ubingwa,” alisema Makoye.

Aliongeza katika sherehe hiyo wanatarajia kupiga mnada vifaa mbalimbali vya michezo kama vile jezi za timu ya wanaume, mipira pamoja na picha za wachezaji nguli wa Simba waliofanikisha kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu uliopita.

Alisema katika kunogesha sherehe hiyo baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza cha timu ya wanaume waliotwaa ubingwa msimu huu watahudhuriwa ikiwa ni kuwapa hamasa dada zao. Timu ya Simba Queens pia watahudhuria.

Makoye alisema mbali na kuchangisha fedha, pia watatumia nafasi hiyo kuzindua tawi lao kwa vile licha ya kuanzishwa mwaka mmoja na nusu uliopita na kuendelea kufanya kazi zake, lilikuwa halijazinduliwa rasmi.

Pia alisema, watatumia sherehe hiyo kuzindua tovuti ya tawi lao ambapo wanatarajia kuendesha mambo yao ya kiofisi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

“Tutatumia nafasi hiyo kuizindua tovuti ya tawi letu…tayari tumeshakamilisha mipango yote na kinachosubiriwa ni hapo keshokutwa Jumapili (kesho) kuitangaza rasmi," alisema mwenyekiti huyo.

Aliongeza, sherehe hiyo itahusisha pia shamrashamara za tawi lao hilo kusherehekea ubingwa kwa timu yao iliyoutwaa msimu huu.

Makoye amewataka wanachama, wapenzi na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi katika sherehe hiyo ili kuwaunga mkono katika jitihada zao za kusaidia kukuza soka kwa klabu yao pamoja na taifa kwa ujumla.   


No comments:

Post a Comment