Sunday, July 8, 2012

SEYDOU KEITA ATIMKA BARCELONA

 *ADAIWA KUVUTIWA NA ‘MIHELA’ CHINA

Si unaona upenyo ule....! Keita akipokea maelekezo ya mwisho kutoka kw Guardiola kabla ya kuingia uwanjani.

Keita (wa pili kushoto) akishangilia goli na wachezaji wenzake wa Barca, kutoka kushoto ni Messi David Villa, Maxwell Scherrer na Dani Alves.

Seydou Keita (kushoto) na Alexis Sanchez wa Barca wakishikilia Kombe la Mfalme baada ya kulitwaa kwa kuifunga Athletic Bilbao kwenye Uwanja wa Vicente Calderon mjini Madrid, Mei 25, 2012.
MADRID, Hispania
Kiungo wa kimataifa wa Mali, Seydou Keita anaondoka Barcelona baada ya kuichezea kwa miaka minne na kutwaa nayo makombe 14.

"Seydou Keita amesema kwamba hataendelea kuichezea klabu hii msimu ujao," Barca walisema kupitia tovuti yao (www.fcbarcelona.com).

"Barcelona inamshukuru Seydou Keita kwa mchango wake katika miaka michache iliyopita na kumtakia mafanikio mema."

Keita, 32, alijiunga na Barca akitokea Sevilla kwa wakati mmoja na kocha Pep Guardiola.

Alikuwa na uhusiano wa karibu na Guardiola na kuondoka kwake kunahusishwa na uamuzi wa kocha huyo kutoendelea kuifundisha Barca baada ya kumalizika kwa msimu uliopita.

Guardiola alimtumia zaidi Keita kama mtokea benchi na kiungo huyo aliisaidia Barca kutwaa mataji matatu ya La Liga (Ligi Kuu ya Hispania), mataji mawili ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na mtaji mawili ya Kombe la Mfalme.

Vyombo vya habari vya Hispania viliripoti kwamba kiungo huyo alikuwa na kipengele katika mkataba wake unaomalizika 2014, kinachomruhusu kuondoka bure ikiwa hataanzishwa katika kikosi cha kwanza katika walau nusu ya mechi za msimu.

Keita amekuwa akihusishwa na uhamisho wa kwenda katika klabu ya Dalian Aerbin inayoshiriki Chinese Super League, Ligi Kuu ya China, ambako huko anatarajiwa kuingia mkataba mnono na kuvuna mabilioni ya pesa kama walivyofanya nyota wengine kadhaa, wakiwemo akina Didier Drogba, Nicolas Anelka na Yakubu Aygbeni.

No comments:

Post a Comment