Thursday, July 5, 2012

PELE: CASILLAS ANASTAHILI TUZO YA MWANASOKA BORA WA DUNIA


Kama nyani vile...! Casillas akifanya vitu vyake wakati wa fainali za Euro 2012 
RIO DE JANEIRO, Brazil
PELE anaamini kwamba sasa ni wakati muafaka kwa kipa Iker Casillas kupewa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia (Ballon d'Or) kufuatia kiwango chake cha juu alichoonyesha wakati akiidakia timu yake ya taifa ya Hispania katika fainali za Euro 2012.

Pele
Nahodha huyo mwenye miaka 32 alienda katika fainali hizo baada ya kuisaidia klabu yake ya Real Madrid kutwaa ubingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania msimu wa 2011-12, na aliruhusu goli moja tu katika fainali za Euro zilizoandaliwa na Poland na Ukraine wakati Hispania ikitwaa tena ubingwa.

Pele anaamini kwamba makipa wamekuwa wakisahaulika katika miongo michache iliyopita wakati akisifia kiwango cha Casillas kwenye michuano mikubwa, na kutaka apewe tuzo hiyo badala ya Lionel Messi.

"Kwa kawaida, ni washambuliaji (wanaopewa tuzo ya Ballon d'Or), lakini mimi naamini haitakuwa sawa kutoa tathmini yangu kwa vile sijaona mechi zote," Pele aliiambia AS.
"Hata hivyo, bado hakuna shaka yoyote kuhusiana na kiwango cha Casillas kwenye michuano mikubwa.  Hii ndio fursa nzuri zaidi, ndio wakati muafaka wa yeye kupewa tuzo ya Ballon d'Or.

"Amechangia kwa ushindi kwa kiasi kikubwa kama walivyofanya washambuliaji. Unaweza kuwa na No.10 bora kabisa, lakini asiwe na msaada wowote kama hakuna kipa bora nyuma nyuma yake.

"Nilikuwa muhimu sana (kwa Brazil), hilo sikatai, ni kwa sababu nilikuwa mshambuliaji. Lakini waangalie (Amadeo) Carrizo, (Lev) Yashin and (Gordon) Banks. Watu hawazungumzii makipa."
  
.... ASIKITIKA LIONEL MESSI KUKOSA MPINZANI
Kushoto kwenda kulia ni Danny Alves na Lionel Messi wa  Barcelona wakiwa na Pele na Neymar wa Santos wakati wa sherehe za kukabidhi tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka 2011 wa Dunia (FIFA Ballon d'Or) mjini Zurich, Uswisi.
Pele pia alizungumzia hali ya sasa ya mchezo wa soka wakati akielezea kukosekana kwa ushindani wa dhati katika ngazi ya Dunia dhidi ya Messi, kabla ya kulaumu vyombo vya habari kwa tabia ya kuzidisha ‘misifa’ kwa wachezaji.
"Kila zama zina nyota wake," alisema.

 "Kuna wakati kunakuwa na wachezaji wanne hadi watano wa kuwalinganisha, lakini kwa mtazamo wangu, sasa hivi hilo halipo.

"Nani leo hii wa kumlinganisha na Messi? Neymar? Cristiano (Ronaldo) ni wa pili, lakini nani mwingine wa kushindana naye?

"Vyombo vya habari nd’o vinavyotengeneza tofauti. Nitapaswa kwenda na kucheza mwezini ili kupata mafanikio niliyowahi kuyapata. Leo, kijana anafunga bao kali na dunia nzima inamtukuza."

No comments:

Post a Comment