Tuesday, July 10, 2012

MOURINHO AFUTIWA ADHABU YA KIFUNGO MECHI YA CLASICO DHIDI YA BARCELONA

Mourinho akiwa kibaruani

MADRID, Hispania
KIFUNGO cha mechi mbili alichopewa kocha Jose Mourinho wa Real Madrid kwa kosa la kumtia kidole cha machoni kocha msaidizi wa Barcelona, Tito Vilanova kimeondolewa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa msamaha wa jumla, Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) lilisema jana.

Uamuzi huo, uliotangazwa kwenye mkutano mkuu wa RFEF mjini Madrid, umeibua uwezekano wa kutokea malumbano kati ya shirikisho hilo na Barca, ambao rais wao Sandro Rosell alisema mwezi uliopita kwamba kamwe hatakubali vitendo vya ukorofi vya Mourinho kuachwa bila kutolewa adhabu.

Kocha huyo mtata raia wa Ureno alifungiwa baada ya kumshambulia Vilanova, ambaye hivi sasa ametwaa mikoba ya ukocha wa Barca kutoka kwa Pep Guardiola, kwa kumfuata kwa nyuma na kumtia kidole cha macho wakati wa mechi yao ya mwisho ya kuwania taji la ‘Super Cup’ msimu uliopita.

Kifungo hicho, ambacho kilitolewa kwa ajili ya Super Cup tu, kiliondolewa na rais wa RFEF, Angel Maria Villar, ambaye alitumia mamlaka yake kusamehe baadhi ya wachezaji na makocha baada ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu.

"Vifungo vya hadi mechi nne na vya mechi mbili kwa uwanja havitatekelezwa," RFEF iliamua, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa ndani ya mkutano.

Uamuzi huo unamaanisha kuwa kufungiwa mechi moja kwa  Vilanova kwa kosa la kujibu mapigo ya Mourinho pia kumefutwa.

Wote sasa wanaweza kuwepo katika mabenchi ya timu zao wakati Real ambao ni mabingwa wa La Liga na Barca waliotwaa Kombe la Mfalme watakapokutana mwezi ujao kuwania Super Cup 2012, mechi mbili za nyumbani na ugenini za kuashiria ufunguzi wa msimu mpya.

Rosell alisema mwezi uliopita kuwa klabu yake itapinga uamuzi wowote ule wa kumsamehe Mourinho.

"Kama akisamehewa (Mourinho), tutazungumza na mamlaka husika, hatutaruhusu aachwe bila kuadhibiwa."

No comments:

Post a Comment