Thursday, July 12, 2012

MNYIKA MATATANI KWA KUSHINDWA KUTHIBITISHA UHUSIKA WA MWIGULU KATIKA WIZI FEDHA ZA EPA


Mhe. Mwigulu (kushoto) akiteta jambo na Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai

Mhe. Mnyika
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) atapelekwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge baada ya kushindwa kuthibitisha tuhuma alizotoa bungeni kuwa Mbunge wa Iramba Magharibi, Mhe. Mwigulu Mchemba (CCM) ni miongoni mwa watu waliohusika na wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).


Akizungumza bungeni leo, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai, alisema kuwa Mnyika aliyekuwa amepewa siku 7 za kuwasilisha ushahidi utakaothibitisha tuhuma za wizi alizotoa dhidi ya Mwigulu, ameshindwa kufanya hivyo.


Kwa sababu hiyo, Mhe. Ndugai akasema kuwa mwongozo wake kuhusiana na suala hilo ni kwamba, atampeleka Mnyika mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ichukue hatua zinazostahili kwa mujibu wa kanuni za Bunge.


Awali, kabla ya kuendelea kwa majadiliano ya makadirio na mapato ya matumizi ya Wizara ya Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Mwigulu alisimama na kuomba mwongozo wa Spika kuhusiana na madai aliyotoa Mhe. Mnyika dhidi yake ndani ya Bunge hilo kuwa yeye (Mwigulu) ni miongoni mwa watu walioiba fedha za EPA (Sh. Bilioni 133) na akatakiwa kuthibitisha  kauli yake ndani ya siku saba lakini hadi leo hajatekeleza jambo hilo ingawa tayari siku alizopewa zimeshapita.


ILIVYOKUWA JULAI 3
 Mnyika alipewa siku saba kuanzia siku aliyotoa kauli hiyo (Julai 3) kuthibitisha tuhuma za wizi wa fedha za EPA alizotoa dhidi ya Mhe. Mwigulu wakati wa kuchangia bajeti ya Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora). Mwenyekiti wa Bunge, Mhe. Jenista Mhagama, ndiye aliyempa agizo hilo baada ya kuibuka majibizano makali wakati Mwigulu akichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.


Awali, Mnyika aliomba mwongozo wa Spika na kupinga baadhi ya maelezo ya Mwigulu ambaye katika mchango wake, aliponda baadhi ya taarifa zilizomo kwenye hotuba ya Waziri Kivuli wa Kambi Rasmi ya Upinzani, ikiwemo iliyodai kuwa hali ngumu ya watumishi wa serikali imewafanya walimu wa shule za msingi kujikuta wakijihusisha na biashara huku wahadhiri wa vyuo mbalimbali vya umma wakilazimika kufundisha pia katika vyuo vingine binafsi hadi vitatu.


Wakati mabishano hayo,  yakiendelea na wakati fulani kuwahusisha wabunge wengine kama Mchungaji Msigwa wa Jimbo la Iringa Mjini (CHADEMA) na Mhe. George Simbachawene wa Kibakwe(CCM), ndipo Mnyika alipomtuhumu Mwigulu kuwa naye ni miongoni mwa watuhumiwa wa kashfa ya fedha za EPA (Sh. bilioni 133) kwani alikuwa ni miongoni mwa watumishi wa Benki Kuu ya Tanzania ambako ndiko wizi huo ulikotokea.


Alisema kwamba inasikitisha kuona kuwa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais (Utawala Bora) haionyeshi ni kwa jinsi gani Idara ya Usalama wa Taifa imekuwa ikizuia uhalifu kama wa EPA. 


Hata hivyo,  Mwigulu aliposimama tena siku hiyo, alianza kwa kusema kuwa wakati wizi wa EPA ukitokea (mwaka 2005), yeye alikuwa bado ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwamba,  (wakati huo) hata mlango wa kuingilia Benki Kuu alikuwa haujui.  Alisema kuwa alianza kazi BoT Oktoba, 2006.

No comments:

Post a Comment