Tuesday, July 3, 2012

MNYIKA APEWA SIKU 7 KUTHIBITISHA TUHUMA ZA WIZI WA FEDHA ZA EPA DHIDI YA MWIGULU

Mhe.John Mnyika

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) amepewa siku saba kuanzia leo kuthibitisha tuhuma za wizi wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) dhidi ya Mbunge wa Iramba, Lameck Mwigulu Mchemba.

Mnyika alitakiwa kufanya hivyo na Mwenyekiti wa Bunge, Mhe. Jenista Mhagama, baada ya kuibuka majibizano makali wakati Mwigulu akichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Utawala Bora).

Awali, Mnyika aliomba mwongozo wa Spika na kupinga baadhi ya maelezo ya Mwigulu ambaye katika mchango wake, aliponda baadhi ya taarifa zilizomo kwenye hotuba ya Waziri Kivuli wa Kambi Rasmi ya Upinzani, ikiwemo iliyodai kuwa hali ngumu ya watumishi wa serikali imewafanya walimu wa shule za msingi kujikuta wakijihusisha na biashara huku wahadhiri wa vyuo mbalimbali vya umma wakilazimika kufundisha pia katika vyuo vingine binafsi hadi vitatu.

Wakati mabishano hayo,  yakiendelea na wakati fulani kuwahusisha wabunge wengine kama Mchungaji Msigwa wa Jimbo la Iringa Mjini (CHADEMA) na Mhe. George Simbachawene wa Kibakwe(CCM), ndipo Mnyika alipomtuhumu Mwigulu kuwa naye ni miongoni mwa watuhumiwa wa kashfa ya fedha za EPA (Sh. bilioni 133) kwani alikuwa ni miongoni mwa watumishi wa Benki Kuu ya Tanzania ambako ndiko wizi huo ulipotokea.

Alisema kwamba inasikitisha kuona kuwa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais (Utawala Bora) haionyeshi ni kwa jinsi gani Idara ya Usalama wa Taifa imekuwa ikizuia uhalifu kama wa EPA. 

Kauli ya kumtuhumu Mwigulu ndiyo iliyomfanya Mwenyekiti (Jenista Mhagama) kumpa siku saba ili athibitishe tuhuma hizo. 

Hata hivyo,  Mwigulu aliposimama tena, alianza kwa kusema kuwa wakati wizi wa EPA ukitokea (mwaka 2005), yeye alikuwa bado ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwamba,  (wakati huo) hata mlango wa kuingilia Benki Kuu alikuwa haujui.  Alisema kuwa alianza kazi BoT Oktoba, 2006.

No comments:

Post a Comment