Monday, July 16, 2012

MBUNGE BADWEL AKANA KUPOKEA RUSHWA

Mbunge wa Bahi, Omary Badwel akielekea mahakamani.


Na Mwandishi Wetu 
MBUNGE wa Jimbo la Bahi, Omary Badwel (43), anayekabiliwa na kesi ya kushawishi na kupokea rushwa ya Sh. milioni 1, amekana mashitaka hayo.

Badwel alikanusha madai hayo wakati akisomewa maelezo ya awali na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Lizy Kiwia, jana.

Mbele ya Hakimu Mkazi Faisal Kahamba, Kiwia, alidai kuwa Mei 30, mwaka huu, mshtakiwa alimpigia simu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya Mkuranga Sipora Liana na kujitambulisha kuwa ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Alidai mshtakiwa alimjulisha Liana kuwa Juni 4, mwaka huu kamati yake itajadili ripoti ya halmashauri hiyo na kwamba mambo sio shwari, ambapo alimtaka kwenda jijini Dar es Salaam, Mei 31, mwaka huu ili wajadili namna ya kumsaidia.

Alidai hata hivyo, Liama, alimjibu mshtakiwa kuwa siku hiyo atahudhuria vikao mbalimbali katika halmashauri yake ambapo alimuahidi kuonana naye Juni Mosi, mwaka huu.

Kiwia aliendelea kusoma maelezo hayo kuwa, siku ya tukio mshtakiwa alimshawishi Liana kutoa rushwa ya Sh. milioni nane ili kamati yake iweze kumsadia kwenye ripoti yake.

Mshtakiwa anadaiwa kuwa akiwa kama Mbunge na Mjumbe wa LAAC na mtumishi wa umma, alitenda kosa hilo kati ya Mei 30 hadi Juni 2, mwaka 2012 jijini Dar es Salaam, hata hivyo mshtakiwa alikana maelezo hayo.

Lakini mshtakiwa alikiri kuwa yeye ni Mbunge wa Bahi na majina ni yake na kuwa ni mjumbe wa kamati ya LAAC.

Alikiri kuwepo na kikao cha kamati yake cha kujadili ripoti za Halmashauri ya Mkuranga na Bagamoyo, Mkoani Pwani Juni 4, mwaka huu.

Mbunge huyo, hata hivyo, alikana mashitaka dhidi yake na yuko nje kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment