Wednesday, July 11, 2012

MARADONA AFUKUZWA UKOCHA AL WASL

Mwanasoka wa zamani wa Argentina, Diego Maradona akiwa na mkewe Veronica Ojeda wakishuhudia mechi ya fainali ya tenisi baina ya Rafael Nadal wa Hispania na Roger Federer wa Uswisi wakati wa fainali za ATP World Tour kwenye Uwanja wa O2 Arena Novemba 28, 2010 mjini London, England.

Mambo magumu... kocha Diego Maradona akipiga hesabu ambazo haziendi.

DUBAI, Muscat
DIEGO Maradona amefukuzwa kazi yake ya ukocha wa klabu ya Al Wasl ya Falme za Kiarabu baada ya kuiongoza kwa miezi 14.

Nafasi ya gwiji huyo Muargentina ilikuwa shakani tangu Juni wakati bodi yote ya klabu  kujiuzulu kufuatia kumaliza msimu bila ya kombe lolote.

Maradona (51), alijiunga na klabu hiyo yenye maskani yake, Dubai Mei 2011 na abado ana mwaka mmoja katika mkataba wake.

Anaondoka baada ya kampeni za kufadhaisha za ligi ambazo ziliishuhudia Al Wasl ikimaliza katika nafasi ya nane kwenye msimamo.

"Kufuatia mkutano wa wakurugenzi wa Al Wasl Football Company uliofanyika kutathmini utendaji wa Al Wasl chini ya uongozi wa kocha Diego Maradona, iliamuliwa kusitishwa kwa mkataba wa kocha Diego Maradona na benchi lake la ufundi," ilisomeka taarifa ya klabu hiyo.

Maradona, mshindi wa Kombe la Dunia akiwa na Argentina mwaka 1986, alitawala vichwa vya habari mwezi Machi mwaka huu wakati alipobwatukiana na mashabiki.

Wakati Al Wasl ilipokumbana na kipigo cha 2-0 katika Ligi Kuu ya UAE ugenini dhidi ya Al Shabab, aliripotiwa kupanda jukwaani kumtetea mkewe baada ya mashabiki kudaiwa kuanza kuwatukana wake za wachezaji.

Maradona aliletwa ili kujaribu kuinua umaarufu wa Al Wasl, kote ndani na nje ya uwanja, hata hivyo walimaliza wakiwa pointi 29 nyuma ya mabingwa Al Ain ya Asamoah Gyan.

No comments:

Post a Comment