Sunday, July 1, 2012

MANAHODHA STARS WANG’ARA TUZO ZA VODACOM

Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye akimsisitiza jambo refa Martin Saanya mara baada ya kumkabidhi tuzo pamoja na kitita cha Sh.Milioni 3.8 ya mwamuzi bora wa ligi kuu ya Vodacom 2011/2012. Anayeshuhudia kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twisa.

Meneja Mahusiano ya Nje wa Vodacom Tanzania, Salum Mwalim (kushoto) na Meneja Mahusiano wa kampuni hiyo Matina Nkurlu wakifuatilia hotuba ya Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kutoa tuzo kwa msimu ulioisha wa ligi kuu ya Vodacom.

NAHODHA wa Taifa Stars, Juma Kaseja na msaidizi wake Aggrey Morris wameng’ara katika hafla ya kampuni ya Vodacom kukabidhi zawadi kwa wachezaji, klabu, waamuzi na makocha waliofanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012.
 
Katika hafla hiyo iliyofanyika jana usiku (Juni 30 mwaka huu) hoteli ya Double Tree Hilton, Dar es Salaam, Morris anayechezea Azam aliibuka mchezaji bora wa ligi hiyo wakati Kaseja anayedakia Simba alikuwa kipa bora.
 
Kila mmoja alizawadiwa Sh. 3,312,500 katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye. Kaseja aliwashinda makipa Mwadili Ally (Azam) na Deogratias Munishi (Mtibwa Sugar) wakati Morris aliwashinda Haruna Niyonzima (Yanga) na Haruna Moshi (Simba).
 
Waziri Mkuu Mstaafu Bw.Frederick Sumaye katikati akishuhudia Mbunge wa Tabora mjini ambaye ni Mwenyekiti wa Simba Sports Club, Aden Rage akipongezwa na Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawasiliano cha Vodacom, Kelvin Twisa mara baada ya kupokea tuzo ya golikipa bora wa mwaka kwa niaba ya Juma Kaseja, wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa msimu ulioisha wa ligi kuu ya Vodacom.

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye katikati akishuhudia Mwenyekiti wa Azam FC, Mohamed Said akipongezwa na Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano cha Vodacom, Kelvin Twisa mara baada ya kupokea tuzo ya mfungaji bora na timu yenye nidhamu na kocha bora kwa niaba ya klabu yake wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa msimu ulioisha wa ligi kuu ya Vodacom iliyoandaliwa na Vodacom Tanzania katika hoteli ya Dobble Tree jijini Dar e Salaam.
 
John Bocco wa Azam aliyefunga mabao 19 ndiye mfungaji bora, refa bora ni Martin Saanya kutoka Morogoro ambaye aliwashinda Oden Mbaga (Dar es Salaam) na Amon Paul (Mara) wakati kocha bora ni Stewart Hall wa Azam aliyewashinda Charles Kilinda (JKT Ruvu) na Charles Mkwasa (Ruvu Shooting). Kila mshindi mepata sh. 3,875,000.
 
Timu yenye nidhamu bora ni Azam iliyopata sh. 7,750,000, mshindi wa tatu Yanga sh. 15,500,000, makamu bingwa Azam sh. 22,000,000 na bingwa Simba sh. 50,000,000.
 
Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye akimkabidhi hundi yenye thamani ya Sh. milioni 15.5 Katibu wa Yanga Selestin Mwesigwa wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa msimu ulioisha wa ligi kuu ya Vodacom iliyoandaliwa na Vodacom Tanzania katika hoteli ya Dobble Tree jijini Dar es Salaam. Anayeshudia katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twisa.
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye (kushoto) akishuhudia Mwenyekiti wa Azam FC, Mohamed Said akipongezwa na Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawasiliano cha Vodacom, Kelvin Twisa mara baada ya kupokea hundi yenye thamani ya Sh. milioni 22 kwa kuibuka washindi wa pili katika msimu 2011/2012 wa ligi kuu ya Vodacom wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa msimu ulioisha wa ligi kuu ya Vodacom iliyoandaliwa na Vodacom Tanzania katika hoteli ya Dobble Tree jijini Dar es Salaam.

Pia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewazawadia sh. 1,000,000 kila mmoja kwa wachezaji watatu vijana wenye umri chini ya miaka 20 waliofanya vizuri kwenye ligi hiyo.
 
Wachezaji hao ambao walikuwa kwenye vikosi vya kwanza vya timu zao ni Frank Domayo (JKT Ruvu), Rashid Mandawa (Coastal Union) na Hassan Dilunga (Ruvu Shooting).

No comments:

Post a Comment