Monday, July 16, 2012

KOVA AKATAA KUMJIBU MCHUNGAJI GWEJIMA KUHUSU MTUHUMIWA WA SAKATA LA DK. STEVEN ULIMBOKA

ASEMA MAHAKAMA ND’O ITAJUA KAMA KWELI MTUHUMIWA NI MGONJWA WA AKILI AMA LA

Kamanda Kova (kushoto) akifafanua jambo.

Dk. Ulimboka akiendelea na matibabu.
Siku moja tu baada ya Mchungaji Gwejima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe jijini Dar es Salaam kupinga maelezo ya Polisi kuhusiana na madai ya kuungama kwenye kanisa lake kwa Mkenya Joshua Mhindi (31) aliyedaiwa kukiri kuwa alishiriki kumteka na kumtesa Dk. Steven Ulimboka; Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ameibuka leo na kusema kuwa kamwe hayuko tayari kmujibu Mchungaji huyo.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kova amesema kuwa hawezi kumjibu Gwejima kwa vile anatambua kuwa suala hilo limeshatua mahakamani na kuendelea kulizungumzia ni sawa na kuingilia uhuru wa mahakama, kitendo ambacho ni ukiukwaji wa sheria za nchi.


Kova ameyasema hayo wakati alipokutana na waandishi wa habari kuzungumzia hali ya uhalifu jijini kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi hadi sasa.


“Najua mnaningoja kwa hamu niizungumzie taarifa iliyotolewa na Mchungaji Josephat Gwejima wa Kanisa la Ufufuo kuhusiana na mtuhumiwa Mhindi… nasema siwezi kuliongelea suala hilo kwa kuwa liko mahakamani na katiba ya nchi inazuia kuzungumzia  suala lililoko kwenye mhimili huo nje ya mfumo wa mahakama. Labda niseme kwamba, ile taarifa ya awali niliyowapatia Julai 13 inabaki kama ilivyo kwa kuwa ina maelezo na ushahidi wote juu ya suala hili,” amesema Kamanda Kova.UGONJWA WA AKILI WA MTUHUMIWA

Hata hivyo, licha ya Kamanda Kova kukataa kuzungumzia kwa undani juu ya taarifa ya Mchungaji Gwejima, aligusia suala alilosema mchungaji (Gwejima) kuwa huenda mtuhumiwa huyo ana matatizo ya akili; akisema kwamba sheria za nchi zinawakumba watu wote wanaotenda makosa ya jinai, wakiwemo wenye matatizo ya akili.


“Kama Mhindi ana matatizo ya akili atapelekwa kwa daktari kwa ajili ya kujua ukweli wa hali aliyokuwa nayo wakati akitenda kosa hili, kama alikuwa ana kichaa kamili, kichaa nusu au la,  mahakama ndiyo inayojua namna ya kushughulika na watu wenye kesi kama hizi,” alisema.


Aliwataka wananchi waendelee kwenda kuungama kwa viongozi wa dini, lakini akaonya kwamba jeshi la polisi kamwe haliko tayari kumuacha mtu aliyekiri mwenyewe kwamba ametenda jinai kwani sheria utachukua mkondo wake.


Jana, wakati wa mahubiri ya ibada ya Jumapili, Mchungaji Gwejima alikana taarifa zilizotolewa na Kamanda Kova kuwa mtuhumiwa Mhindi ambaye ni raia wa Kenya alienda kanisani kwao kuungama na kukiri kwamba alishiriki kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka kwa kushirikiana na wenzake wa kikundi cha Kenya cha Gun Star.

Hivi sasa, Dk. Ulimboka ambaye ni kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini. Alikuwa mstari wa mbele wakati wa mgomo wa madaktari uliofanyika hivi karibuni na katikati ya mgogoro huo akakumbwa na kadhia ya kutekwa na watu wasiojulikana, akapigwa na kuteswa vibaya kabla ya kutupwa katika msitu wa Mabwepande jijini Dar es Salaam. 

 

No comments:

Post a Comment