Sunday, July 8, 2012

KINONDONI, DODOMA ZAINGIA ROBO FAINALI COPA

TIMU za Kinondoni na Dodoma zimeingia robo fainali ya michuano ya Copa Coca Cola 2012 baada ya kushinda mechi zao za 16 bora zilizochezwa leo jijini Dar es Salaam.
 
Kinondoni imeitoa Rukwa baada ya kuichapa mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Karume. Mabao ya washindi yalifungwa na Yahya Mohamed dakika ya 13, Issa Allydakika ya 44 na Mabrouk Liyayala dakika ya 80. Ladislaus Fwamba aliifungia Rukwa dakika ya 46.
 
Kwa ushindi huo, Kinondoni itacheza robo fainali ya tatu Julai 10 mwaka huu Uwanja wa Karume dhidi ya mshindi wa mechi ya 16 bora kati ya Kilimanjaro na Mwanza itakayochezwa leo saa 10 jioni.
 
Nayo Dodoma imenyakua tiketi ya kucheza robo fainali baada ya leo kuifunga Arusha bao 1-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers. Bao la washindi lilifungwa dakika tano kabla ya filimbi ya mwisho na Ayoub Khalfan.
 
Katika robo fainali, Dodoma itacheza na mshindi wa mechi ya 16 bora kati ya Tabora na Tanga itakayochezwa leo jioni Uwanja wa Tanganyika Packers.
 
Robo fainali zote zitachezwa Uwanja wa Karume ambapo ya kwanza itafanyika keshokutwa asubuhi (Julai 10 mwaka huu) kati ya Temeke na Mjini Magharibi wakati jioni itakuwa Mara na Morogoro.
 

No comments:

Post a Comment