Monday, July 9, 2012

KAMATI MISS TZ KUTEMBELEA REDDS MISS SINZA 2012 KESHO

Warembo wa Redds Miss Sinza wakiwa mazoezini kwenye ukumbi wa Mawela Social (Ten Star Lounge) uliopo karibu na hotel ya Vatican chini ya mwalimu wao Mwajabu Juma (kulia) ambaye anashikiria taji la Top Model. Warembo hao watapanda jukwaani Julai 13 kutafuta tiketi ya kuiwakilisha Sinza katika mashindano ya Kanda ya Kinondoni na baadaye Miss Tanzania. Picha: Mpigapicha Wetu
      
Na Mwandishi Wetu
WAKATI bendi ya African Stars (Twanga Pepeta) itapamba shindano la kumsaka mrembo wa Redds Miss Sinza 2012 lillopangwa kufanyika Ijumaa kwenye ukumbi wa Mawela Social (Ten Star Lounge) uliopo karibu na hotel ya Vatican City, Kamati ya Miss Tanzania kesho itatembelea warembo hao kwa lengo la ‘kuwafunda’  tayari kupanda jukwaani.


Mratibu wa kampuni ya Calapy Entertainment, Majuto Omary alisema jana kuwa Twanga Pepeta imeandaa zawadi kwa mashabiki wake na wa urembo kwa kuwapa uhondo wa nyimbo mbili mpya zitakazokuwa zinasikika kwa mara ya kwanza jukwaani.


Nyimbo hizo ni "Mapambano ya Maslahi" uliotungwa na Muumin Mwinjuma, "Shamba la Twanga" ambao umetungwa na Greyson Semsekwa na mmoja ambao haujapewa jina uliotungwa na Jumanne Saidi ambaye amefunga ndoa na mnenguaji wa bendi hiyo, Asha Sharapova.


Alisema kuwa nyimbo hizo ni zawadi kwa mashabiki wa Twanga wa Sinza na vitongoji  vyake kwani bendi hiyo haijafanya shoo eneo hilo kwa muda mrefu.


"Tunatarajia kuwa na shoo nzuri kutoka kwa warembo na bendi ya Twanga Pepeta ambayo mwaka huu imeshinda tuzo mbili katika tuzo za muziki Tanzania," alisema.


Kuhusiana na ziara ya Kampuni ya Lino International Agency, Majuto alisema kuwa Lundenga na wenzake watafanya mazungumzo na warembo hao baada ya mazoezi yao ya pamoja.


Alisema kuwa ziara hiyo ni faraja kwa warembo na kamati ya Miss Sinza ambayo shindano lake ndilo linalohitimisha mashindano ya vitongoji nchini.


"Miss Sinza ndiyo inafunga pazia la mashindano ya vitongoji (vituo) nchini, Lundenga na wenzake wanakuja kutoa baraka zao kabla ya kuanza pilikapilika za Redds Miss Tanzania," alisema.


Shindano hilo linadhaminiwa na Redds Premium Cold, Dodoma Wine, Kidoti Fashion, Clouds Entertainment, sufianimafoto.blogspot.com, Lady Pepeta na flexi P, Fredito Entertainment, Screen Masters, Brake Point na Jackz Cosmetics Kinondoni.

--------------

No comments:

Post a Comment