Thursday, July 12, 2012

JAJI AIWEKA NJIA PANDA NDOA YA DK. SLAA NA JOSEPHINE MUSHUMBUZI ILIYOPANGWA KUFUNGWA JUMAMOSI IJAYO


Dk. Slaa (kulia) akiwa jukwaani na mchumba wake Josephine Mushumbuzi

Dk. Slaa akiwa na Rose Kamili
Ile ndoa kati ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa na mchumba wake Josephine Mushumbuzi iliyopangwa kufanyika Jumamosi ijayo (Julai 21) sasa iko njia panda baada ya Jaji Lawrance Kaduli wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam anayesikiliza pingamizi la ndoa hiyo lililowekwa na aliyekuwa mke wa Dk. Slaa, Rose Kamili kuamuru kuwa suala hilo lifikishwe tena kortini Agosti 14,  ikiwa ni baada ya kupita kwa tarehe iliyopangwa kwa ajili ya kufungwa kwa ndoa hiyo.


Mahakama hiyo imepanga kuwa Agosti 14 mwaka huu isikilize kesi hiyo ya kusimamisha ndoa ya Katibu  Mkuu wa Chadema, Dk. Willibroad Slaa na mchumba wake Josephine Mushumbuzi inayotarajiwa kufungwa katika wilaya ya Karatu mkoani Manyara. 


Jaji Kaduli, leo ameitaja kesi hiyo namba 4 ya mwaka 2012, iliyofunguliwa na mke wa Dk, Slaa,  Rose Kamili ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema). Jaji huyo aliwataka Dk Slaa na Josephine wajibu pingamizi  hilo la ndoa yao kwa njia ya maandishi kabla ya Julai 30, mwaka huu. 


Pia alimtaka Rose Kamili kupitia wakili wake, Joseph Thadayo kama watakuwa na majibu yoyote wayafaili Agosti 7, mwaka huu na kwamba baada ya taratibu hizo kufanyika, Agosti 14 mwaka huu ataisikiliza kesi hiyo.
Kwa maana hiyo, ndoa hiyo iliyotajiwa kufungwa Jumamosi ijayo ya Julai 21, haitafungwa hadi hapo Mahakama Kuu itakapotoa maamuzi juu ya maombi hayo.
Katika kesi hiyo dhidi ya Dk Slaa na  mchumba wake Josephine Mushumbusi, mlalamikaji Rose Kamili anaiomba Mahakama kusimamisha ndoa hiyo iliyopangwa kufungwa wilayani Karatu mkoa wa Manyara. 


Rose pia anaiomba mahakama imuamuru Dk. Slaa kumlipa Sh. milioni 50 kama fidia aliyotumia kujihudumia pasipo matunzo ya mumewe huyo.
Mbunge huyo kupitia wakili wake Thadayo, anaiomba pia mahakama iamuru Mushumbuzi amlipe Sh. milioni 500 kama fidia ya maumivu aliyoyapata kutokana na kitendo chake cha kuingilia ndoa yao.
Katika hati hiyo ya madai, mbunge huyo anadai kuwa ndoa inayotarajiwa kufungwa kati ya Dk.Slaa na Mushumbuzi ni batili kwa sababu kuna ndoa nyingine halali na inayoendelea kuishi kati ya Dk. Slaa na yeye (Rose Kamili) iliyofungwa mwaka 1985. 


Alidai baada ya kufugwa kwa ndoa hiyo, Juni 18 mwaka 1987 walifanikiwa kupata mtoto wa kike anayeitwa Emiliana na baadaye  Septemba 23  mwaka 1988, walipata mtoto mwingine wa kiume aitwaye Linus Amsi.
Katika uhusiano wao, Dk. Slaa akiwa ni Padri wa Kanisa la Roman Katoliki, alifanya taratibu zilizomwondosha katika nafasi hiyo ya upadre na kuanza maisha ya familia.
Baada ya taratibu hizo, jamii ya Watanzania iliwatambua kama mume na mke ambapo hata kumbukumbu za hati za kimataifa kama za kusafiria ziliwatambua wao kuwa ni wanandoa. 


Rose Kamili aliendelea kudai katika maelezo hayo kuwa yeye na Dk. Slaa waliishi maisha ya ndoa yenye amani, yaliyowawezesha kupata mali kadhaa walizomiliki kwa pamoja ikiwemo nyumba iliyopo kwenye kiwanja namba 609 kitalu E, nyumba ya makazi iliyopo kijiji cha Gongali huko Karatu na vifaa mbalimbali vya nyumbani. 


Hati ya mashtaka imeendelea kueleza kuwa, uhusiano kati ya Slaa na mkewe  Kamili, ulianza kuharibika  mwaka  2009, baada ya  Slaa kuwa na mahusiano  na mwanamke mwingine kinyume  cha sheria. "Tangu mwaka huo 2009, Slaa akaitelekeza familia yake kwa kutoipatia huduma," imeeleza hati hiyo. 


Kamili anaiomba  mahakama iamuru kuwa yeye na Slaa bado ni mke na mume na kwamba Mushumbusi aliingilia ndoa yao hivyo mahakama izuie ndoa inayotajiwa kufungwa  Julai 21, mwaka huu huko Karatu mkoani Manyara.
Kamili pia amewasilisha hati hiyo ya mashtaka kwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo. 


Kamili akamweleza askofu mkuu huyo wa jimbo Katoliki la Dar es Salaam, kuwa moja ya Parokia za Dar es Salaam zina taarifa ya ndoa hiyo.
Nakala ya madai hayo pia imewasilishwa kwa msajili wa Mahakama Kuu, Msajili wa ndoa na kwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Mbulu.

No comments:

Post a Comment