Tuesday, July 3, 2012

HATUJAIKIMBIA SIMBA ZANZIBAR - MINZIRO

Kocha Fred Felix Minziro akisimamia mazoezi ya Yanga kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama leo asubuhi. Picha: Amur Hassan
Athumani Iddi 'Chuji' akigangwa baada ya kuumia katika mazoezi ya Yanga kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama leo asubuhi. Picha: Amur Hassan

Haruna Niyonzima akiwa katika mazoezi ya Yanga kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama leo asubuhi. Picha: Amur Hassan
Hamis Kiiza (Katikati) akiwania mpira dhidi ya Oscar Joshua (kulia) wakati wa mazoezi ya Yanga leo asubuhi Kijitonyama. Picha: Amur Hassan
Chezea jua la Bongo? Hapa sio Vancouver, Canada.... 'Jembe jipya' Nizar Khalfan akipoza koo kwa maji wakati wa mazoezi ya Yanga leo asubuhi kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama. Picha: Amur Hassan
Mshambuliaji Hamis Kiiza (kulia) akifanya utani na kufurahi pamoja na wachezaji wenzake wa Yanga, Kelvin Yondani (kushoto) na Jerryson Tegete wakati wa mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama leo asubuhi. Picha: Amur Hassan
Kelvin Yondani (wa pili kushoto) akiwa na kocha Minziro (kushoto) na wenzao wakati wa mazoezi ya Yanga asubuhi ya leo.


Na Amur Hassan, Kijitonyama
KOCHA wa Yanga, Fred Felix Minziro, amesema sababu ya kupeleka timu B katika michuano ya Urafiki inayoendelea Zanzibar si kuwahofia mahasimu wao Simba.

Yanga walilala 5-0 katika mechi ya mwisho kukutana na mahasimu wao wa Msimbazi na kumekuwepo na minong'ono kwamba kitendo cha mabingwa wa Kombe la Kagame kutopeleka timu A Zanzibar kinalenga kukwepa aibu nyingine kubwa.

Hata hivyo, akizungumza na STRAIKA muda mfupi uliopita wakati wa mazoezi ya Yanga kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama, Minziro amesema hawajawahi kuwahofia Simba.

"Tumekuwa na muda mfupi sana wa mazoezi ya pamoja. Tumecheza mechi moja ya kujipima dhidi ya Express (ya Uganda ambayo wana Jangwani walishinda 2-1) na tunahitaji muda zaidi wa kufanya mazoezi ya pamoja.

"Tumefanya mazoezi kwa wiki mbili tu kisha twende tukacheze mechi tano zenye kupumzika siku moja-moja, halafu kuna michuano ya Kagame inakuja Julai 14. Huwezi kwenda namna hiyo. Tunahitaji mazoezi. Tunahitaji kutetea kombe," alisema nyota huyo wa zamani wa klabu hiyo.

Katika mazoezi hayo yaliyomalizika saa sita mchana, nyota wote wa Yanga walikuwepo.     

Kiungo wa timu ya taifa ya Rwanda, Haruna Niyonzima, Mganda Hamisi Kiiza, beki aliyejiunga kutoka Simba, Kelvin Yondani, Nizar Khalfani, wote walifanya mazoezi ya pamoja huku kipa Yaw Berko ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, naye alisimama langoni akipangua mashuti kama "kawa" akithibitisha kuwa yuko fiti kabisa.

Minziro alisema Yanga itaendelea na mazoezi katika uwanja huo kesho asubuhi.

No comments:

Post a Comment