Thursday, July 12, 2012

GIZA TOTORO LAMLAZIMISHA SPIKA KUAHIRISHA KIKAO CHA BUNGE

Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai

Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai amelazimika kuahirisha kikao cha Bunge kilichokuwa kikiendelea jioni hii hadi kesho saa 3:00 asubuhi baada ya taa zote za ndani ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma kuzimika ghafla na kusababisha giza kubwa kiasi cha kuibua hofu.

Tukio hilo limetokea wakati Bunge lilipokaa kama kamati ili kupitisha vifungu vya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Baada ya taa hizo kuzimika, Mhe. Ndugai akalazimika kuahirisha zoezi lililokuwa likiendelea la kupitisha vifungu na Bunge likarejea katika hali yake ya kawaida kabla naibu spika huyo hajatoa hoja ya kuahirisha kikao hicho hadi kesho asubuhi.

Kabla ya hapo, tayari wabunge walishaanza vituko kwa kupeana vijembe gizani, baadhi wakiwaita wenzao kuwa ni “wanafiki” na wengine wakituhumiana kwa utani juu ya madai kwamba wamefanya hujuma ili kutibua kikao hicho.


No comments:

Post a Comment