Sunday, July 8, 2012

EPIQ BONGO STAR SEARCH YAPATA WAKALI ARUSHA

Jaji Mkuu Madame Ritha (aliyesimama) 'akipasua' kichwa pamoja na majaji wenzake Master Jay (kushoto) na Salama J (kulia) katika kuamua washindi wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Epiq Bongo Star Search mjini Arusha.

Majaji wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Epiq Bongo Star Search, Master Jay (kushoto), Jaji Mkuu Ritha Paulsen (katikati) na Salama Jabir (kulia) wakifuatilia kwa makini vijana wakifanya vitu vyao mjini Arusha.

Vijana wakipanga foleni kusubiri kuingia kuonyesha "maujuzi" yao mbele majaji wakati wa shindano la Epqiq BSS Arusha.

Mh! Mbona kila mtu mshindi? Majaji wakijiuliza wakati wa shindano la Epiq BSS Arusha

Na Mwandishi Wetu
PAZIA la mchujo wa kusaka vipaji vya wawakilishi wa mkoa wa Arusha katika fainali za EBSS 2012 lilifungwa rasmi jana katika ukumbi wa Triple A.


Siku mbili za usindani mkali, ulioleta pamoja zaidi ya vijana 800 kugombea nafasi ya kuwakilisha Arusha, zilikuwa ngumu kwa majaji kuamua washindi.


Mbali na vijana wengi wa Arusha kupenda zaidi kuimba nyimbo za Hip Hop huku mkoa huu ukisifika zaidi kuwatoa wasanii wengi wa muziki huo, katika shindano hilo ilikuwa ni tofauti kwa kuwa wasanii wengi waliamua kuimba.


Jaji Mkuu wa EBSS 2012, Ritha Paulsen alikiri kuwa katika mikoa ya Lindi, Dodoma na kisiwa cha Zanzibar ambapo walienda kusaka vipaji kwa Arusha hali imekuwa nzuri zaidi.


“Najua kila mkoa ambao tulienda tuliona upekee wake na kila mkoa ulikuwa na ladha yake, kwa Arusha tumekuta kuwa kuna hata walio na umri wa chini ya miaka 17 wamekuja wengi na wamefanya vema," alisema Ritha.


Aliongeza kuwa kadri miaka inavyozidi kwenda mbele ndivyo shindano hilo linavyozidi kupanda chati hasa kwa hamasa inayozidi kujionyesha kati ya vijana.


"Mbali na kuwachagua wale ambao wanakuwa wana vipaji lakini pia kuna wakati huwa tunatoa elimu au ushauri wa bure kwa washiriki hawa, kuna wengine wanaonekana kuwa wanaweza kuigiza na pia kufanya sanaa nyingine hivyo tunawashauri nini cha kufanya," aliongeza Madam Ritha.


Akizungumzia shindano hilo, Mkurugenzi wa Masoko wa Zantel, Deepak Gupta, anasema amefurahishwa na vijana wengi waliojitokeza, na anafurahi Zantel kuwa sehemu ya kuwasaidia vijana hao kufikia ndoto zao.


"Vijana waliojitokeza wanaonyesha kuwa wanahitaji msaada, na ndio maana mwaka huu tumeanzisha kampeni kwenye mitandao ya kijamii ili kuwatengenezea fursa vijana hao hata wasipochaguliwa," alisema Gupta.

No comments:

Post a Comment