Tuesday, July 17, 2012

EL CLASICO YA REAL MADRID, BARCELONA YARUDISHWA NYUMA KUPISHA TUZO UEFA


Nyota anayetetea Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Ulaya, Lionel Messi.
MADRID, Hispania
MECHI ya marudiano ya taji la Hispania la ‘Super Cup’ kati ya Real Madrid na Barcelona imerudishwa nyuma kwa siku moja baada ya kubainika kuwa nyota 11 wa klabu hizo wamo katika orodha ya wanaowania Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Ulaya itakayotolewa Agosti 30. 


"UEFA imeliomba Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) kubadili tarehe ya mechi ya marudiano ya kuwania Super Cup, kutoka Agosti 30 na kuwa 29," RFEF imesema kupitia taarifa yake ya leo. 


"..ni ili mechi hiyo isiingiliane na hafla ya utoaji tuzo iliyopangwa na shirikisho la soka la Ulaya kufanyika siku hiyo mjini Monaco." 


Mechi ya kwanza ya Super Cup ambayo huashiria mwanzo wa msimu mpya wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania, kati ya Barca ambao ni mabingwa wa Kombe la Mfalme na Real wanaoshikilia ubingwa wa La Liga, itachezwa Agosti 23 kwenye Uwanja wa Nou Camp na marudiano yatafanyika kwenye Uwanja wa Bernabeu katika wiki inayofuata. 


Wachezaji wa Real, Xabi Alonso, Iker Casillas, Fabio Coentrao, Mesut Ozil, Pepe, Sergio Ramos na Cristiano Ronaldo ni miongoni mwa nyota 32 wanaowania tuzo hiyo, sambamba na wakali wanne wa Barca ambao ni Cesc Fabregas, Andres Iniesta, Xavi na anayeshikilia tuzo hiyo kwa sasa, Lionel Messi.

No comments:

Post a Comment