Tuesday, July 17, 2012

CASILLAS HAJUI TUZO BALLON D'OR AMPE RONALDO, MESSI


Iker Casillas akiwa kazini

Iker Casillas akiangalia wapi auanzishe mpira baada ya kuudaka
MADRID, Hispania
KIPA Iker Casillas (31) ametajwa kuwa ni miongoni mwa nyota wanaostahili kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia (FIFA Ballon d'Or) baada ya kuiongoza Hispania kutwaa ubingwa wa Euro 2012 na pia kuiongoza klabu yake ya Real Madrid kutwaa taji la La Liga, Ligi Kuu ya Hispania.

Hata hivyo, mwenyewe anasema hajui ni nani ampigie kura ya kutwaa tuzo hiyo, licha ya ukweli kwamba mchezaji mwenzake wa Real, Cristiano Ronaldo pia ni miongoni mwa nyota wanaowania tuzo hiyo, sambamba na straika Lionel Messi anayeitetea kwa mara ya nne mfululizo.

"Ninapaswa kufanya uchambuzi wa kina… ni uamuzi mgumu kwa sababu kuna wachezaji wengi ambao ni wazuri sana,” Casillas aliwaambia waandishi wa habari mjini Caracas.

"Hata hivyo, nina muda wa kutosha kufikiria juu ya suala hilo kwani kura hazitapigwa hadi Desemba."

Casillas amekataa kujipa matumaini ya kutwaa tuzo hiyo binafsi yenye hadhi ya juu zaidi katika mchezo wa soka kwa sasa, lakini amekiri kwamba anajiona mwenye furaha kubwa kwa kutajwa katika orodha ya wanaowania tuzo hiyo na kuwawakilisha makipa wa kila mahala.

"Watu wengi wanafurahia kuona makipa nyota wakiruka vizuri na kuokoa," aliongeza, akizingatia ukweli kwamba kwa kawaida, tuzo hiyo huwapa nafasi zaidi mastraika na viungo washambuliaji.

No comments:

Post a Comment