Tuesday, July 3, 2012

CASILLAS ALIMWOMBA REFA AMALIZE MECHI WASIWADHALILISHE ITALIA

Kipa Iker Casillas (kushoto) wa Hispania akijinyoosha kuokoa mpira mbele ya mchezaji mwenzake Sergio Ramos (katikati) na Mario Balotelli wa Italia huku mwamuzi wa "nyuma" ya goli akishuhudia wakati wa mechi yao ya fainali ya Euro 2012 kwenye Uwanja wa Olimpiki Julai 1, 2012 mjini Kiev, Ukraine. Casillas alimwomba mwamuzi wa "nyuma" ya goli awasiliane na refa wamalize pambano wasiwadhalilishe Italia.

WAKIONGOZA kwa magoli 4-0 dhidi ya wachezaji 10 wa Italia katika mechi yao ya fainali ya Euro 2012, nahodha wa timu ya taifa ya Hispania, Iker Casillas alifanya wapinzani wake washindwe kumchukia kwa kuwaomba waamuzi wamalize mpira kabla ya dakika tatu za majeruhi hazijamalizika.

Casillas, ambaye amekuwa mchezaji wa kwanza kabisa katika historia kupata ushindi katika mechi 100 za kimataifa na kuweka rekodi ya kucheza dakika 509 bila ya kuruhusu goli katika michuano hiyo (akiipiku rekodi iliyopita ya Muitalia Dino Zoff ya dakika 494), kufuatia ushindi huo wa fainali, alimuita mwamuzi msaidizi (wa "nyuma" ya goli) na kumwambia, "Waheshimu wapinzani." "Waheshimu Italia," alirudia wakati wachezaji wenzake wakiwa na mpira katika nusu ya Italia wakisaka kufunga bao la tano.

Kisha katika kusisitiza, alisema kwa sauti kuwa magoli hayo yanatosha. Wakati akisema hivyo, refa akapuliza firimbi ya mwisho mara moja baada ya ombi hilo la Iker, lakini bila ya Casillas kutambua, dakika zote 93 zilikuwa zimeshamalizika.

Casillas kisha akampa mkono mwamuzi aliyekuwa akizungumza naye kabla ya sherehe za Hispania kuanza.

Lilikuwa ni jambo dogo lililomaliza kimya, lakini pointi iko pale pale kwamba alionyesha uanamichezo wa kweli. Hivyo, mheshimuni "Mtakatifu" Iker.

No comments:

Post a Comment