Wednesday, July 18, 2012

BOTI ILIYOZAMA ZANZIBAR: WALIOOKOLEWA WAKIWA HAI WAFIKIA 145, UOPOAJI WA MAITI BAHARINI WAENDELEA


Askari wakisaidiana kubeba maiti mmojawapo aliyeopolewa baharini baada ya kuzama kwa boti ya Skagit. Hapa ni kwenye bandari ya Zanzibar. 

Baadhi ya wananchi na askari wakiwa na nyuso za huzuni bandarini Zanzibar kusubiri ujio wa maiti zaidi kutoka katika boti iliyozama leo ya Skagit.

Zoezi la utoaji wa maiti zilizoopolewa likiendelea baada ya kuzama kwa boti ya Skagit.

Add caption

Wananchi wakiwa bandarini Zanzibar kujaribu kutambua ndugu na jamaa zao waliokuwamo katika boti iliyozama leo ya Skagit.

Wanajeshi wakijipanga jioni hii tayari kwa zoezi la kubeba maiti zilizoopolewa baharini baada ya kuzama kwa boti ya Skagit.(Picha:Kwa hisani ya sufianimafoto.blogspot.com)

Boti ya Skagit ilivyokuwa baada ya kupigwa na wimbi kali eneo la Chumbe leo kabla ya kuzama yote baharini.
Taarifa za usiku huu kutoka Zanzibar zimeendelea kudai kuwa hadi sasa, watu waliookolewa wakiwa hai bado ni 145 tu na pia maiti 14 zimeopolewa huku abiria wengine kadhaa kati ya wanaokadiriwa kufikia 250-300 waliokuwamo ndani ya boti ya Skagit iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Zanzibar wakihofiwa kuzama.


Hivi sasa, boti hiyo iliyokumbwa na ajali katika eneo la Chumbe imezama kabisa na haionekani tena kama ilivyokuwa awali; huku juhudi zaidi za kuokoa abiria waliokuwamo zikiendelea kufanyika, ingawa ni kwa shida kwani hali ya bahari katika eneo la tukio si shwari.


Maelfu ya watu waliotaharuki visiwani Zanzibar wamekuwa wakikimbilia katika eneo la viwanja vya Maisara ambako turubai kubwa limefungwa.

Watu wamejazana Maisara kujaribu kutambua ndugu na jamaa waliokumbwa na ajali hiyo, huku vikosi vya uokoaji vikifikisha miili ya marehemu kila inapoopolewa baharini.

Kwa mujibu wa manusura wa ajali hiyo, ni kwamba boti waliyopanda ilianza kuzama baada ya kupigwa na wimbi kali na kupinduka.


Hadi sasa, hakuna taarifa zozote rasmi zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuhusiana na ajali hiyo. Tukio hilo  limetokea takriban mwaka mmoja tu tangu ajali nyingine ya kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders kwenye eneo la Nungwi kuua watu zaidi ya 2,000 wakati ikitokea Zanzibar kuelekea Pemba huku ikiwa imejaza watu kupita kiasi. 

No comments:

Post a Comment